Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
12 February 2026, 8:21 pm

Pamoja na mambo mengine Jeshi la Polisi limeendelea kuikumbusha jamii kutotelekeza familia zao kwani hali hiyo inaathiri malezi ya watoto
Na Katalina Liombechi
Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi “Police Family Day” yanayofanyika Februari 13, kila mwaka, Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero leo limefanya matendo ya huruma kwa kumtembelea mama mwenye watoto mapacha watatu aliyetelekezwa na mumewe katika eneo la Mahutanga, Kata ya Lumemo.
Jeshi hilo limemkabidhi msaada wa chakula pamoja na vifaa vya ujenzi (mchanga na saruji) kwa ajili ya kuboresha makazi yake ambapo pamoja na mambo mengine Jeshi la Polisi limeendelea kuikumbusha jamii kutotelekeza familia zao kwani hali hiyo inaathiri malezi ya watoto.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kilombero, OCD Daud Nkuba, amesema ni utamaduni wa Jeshi la Polisi kuwa karibu na jamii kwa kushirikiana katika ulinzi na usalama pamoja na kufarijiana katika nyakati za mahitaji.
Aidha, familia ya Polisi Kilombero imemtembelea na kumfariji mtumishi mwenzao, Afande Julius, aliyekuwa akiugua, na kumpatia msaada wa mahitaji ya chakula.

Christina Lishela mama wa mapacha watatu ,Diwani wa kata ya Lumemo pamoja mwananchi wa eneo hilo wameelezea kushukuru kwa msaada uliotolewa na jeshi la polisi kwa wahitaji huku wakiahidi kulipa ushirikiano Jeshi hilo katika masuala ya ulinzi na usalama.

Maadhimisho ya Police Family Day hufanyika kila mwaka Februari 13 ambapo Kwa mwaka 2026, yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Polisi Jamii, Rejesha Amani na Utulivu”, na katika Wilaya ya Kilombero yanatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Kiungani.”