Pambazuko FM Radio

Mil 2 yasaidia chakula kwa watoto yatima Mlimba

24 December 2025, 7:28 pm

Picha ya Jamal Idrisa Mkurugenzi wa Mlimba akikabidhi Msaada kwa watoto(Picha na Kuruthumu Mkata)

Watoto yatima na wenye mahitaji maalum bado ni jukumu la jamii kuhakikisha mahitaji mbalimbali

Na Katalina liombechi/Kuruthumu Mkata

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba amekabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mbalimbali wenye thamani ya shilingi milioni 2 kwa watoto yatima wanaolelewa katika Kituo cha Malezi cha Mbingu Sisters, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum ndani ya siku 100 za kipindi cha uongozi wake.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Desemba 24, 2025, Mkurugenzi huyo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajali watoto yatima na wenye mahitaji maalum, kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya maisha na malezi bora.

Ameeleza kuwa lengo la kutoa msaada huo wa chakula na mahitaji mengine ni kuwawezesha watoto hao kufurahia sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kama watoto wengine, sambamba na kuwapatia faraja na matumaini ya maisha bora.

Pamoja na Mambo mengine Ndugu Jamal ameikumbusha jamii kuwakumbuka watoto hao ambao ni faida kwa jamii nzima watakapokuwa viongozi na watu wema hapo baadae.

Picha ya Mkurugenzi Jamal Katikati,kushoto ni Diwani na kulia ni Sister Maria wakiwa na watoto(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya DED Mlimba

Kwa upande wake Sista Mlezi Maria Sapiencia katika kituo hicho kwa niaba ya Uongozi wa kituo cha Mbingu Sisters wameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kwa msaada huo, wakieleza kuwa utawasaidia kwa kiasi kikubwa katika malezi na ustawi wa watoto waliopo kituoni hapo.

Sauti ya Sista Mlezi