Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
2 December 2025, 9:47 pm

Inapofikia maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu wadau wanahimizwa kuendelea kuwekeza katika huduma jumuishi ili kuhakikisha kuwa watu wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata huduma bora na stahiki bila vikwazo.
Na Katalina Liombechi
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, Desemba 3, 2025 changamoto ya upatikanaji wa huduma shirikishi kwa watu wenye ulemavu bado inaendelea kuonekana katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na Pambazuko FM, Elizabeth Luta kupitia kwa mkalimani Mwalimu Ngewe kutoka Chama cha Viziwi Wilaya ya Kilombero, amesema watu wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakikumbana na ugumu mkubwa wanapohitaji huduma katika taasisi mbalimbali kutokana na ukosefu wa wataalam wa lugha ya alama.
Amesema wanapotembelea hospitali, ofisi za umma au sehemu nyingine za huduma, mara nyingi hushindwa kuelewana na wahudumu, jambo linalowafanya kukosa haki zao za msingi na kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Freedom Crispine Lugongo, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na nyinginezo zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Ameeleza kuwa halmashauri tayari imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo, ikiwemo kutumia lugha ya alama.

Aidha Afisa ustawi huyo amesema licha ya kushirikiana na wadau mbalimbali,kama Halmashauri wamekuwa na bajeti ya kuwainua watu wenye ulemavu kiuchumi,kuwatambua na kuwafikia kwa huduma mbalimbali wanafunzi na hata walio nje na shule huku akitoa wito kujiunga katika vyama vya watu wenye ulemavu ili wawe na sauti ya pamoja.
Maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu 2025 kimkoa yanafanyika Morogoro Mjini yanakwenda na kauli mbiu isemayo “Kuendeleza jamii jumuishi kwa watu wenye ulemavu kwa mustakabali wa ustawi na jamii’’