Pambazuko FM Radio

Wasimamizi wa uchaguzi Ifakara wajengewa uwezo

26 October 2025, 2:28 pm

Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura (Picha na Kuruthumu Mkata)

“Uchaguzi ni Mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria ambazo hupaswa kufuatwa hatua hizo ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki”

Na Katalina Liombechi

Wasimamizi wa vituo kutoka kata 19 katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Jimbo la Kilombero mkoa wa Morogoro wamepatiwa mafunzo na kula kiapo cha uaminifu na uadilifu kabla ya kusimamia zoezi la upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia leo Oktoba 26,2025 katika ukumbi wa Mlimba Ifakara yanalenga kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa uzingatifu wa sheria, uwazi na haki, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na bila ya upendeleo.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo Bi Joha Mlindwa ametaja kwa idadi wasimamizi wa Vituo luwa ni 597,Wasimamizi wasaidizi wa vituo ni 1964 watakaofanya shughuli za uchaguzi katika vituo 597 vilivyopo ndani ya kata 19 za Halmashauri ya mji wa Ifakara.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Msimamizi huyo wa Uchaguzi amewasisitiza wasimamizi hao wa vituo,kuwa waaminifu na kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya vyama au watu binafsi huku akiwataka kutokuwa chanzo cha malalamiko,kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalum kama wajawazito,wazee na watu wenye ulemavu.

Picha ya Joha Mlindwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Joha Mlindwa

Baadhi ya Wasimamizi hao wamesema wameyapokea mafunzo hayo na kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kiapo chao.

Picha ya Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura

Nchini Tanzania Zoezi la upigaji kura linatarajiwa kufanyika Octoba 29,2025 ambapo wananchi watapata fursa ya kuwachagua viongozi wao wa ngazi mbalimbali kuanzia Rais,Mbunge na Diwani na kauli mbiu ya mwaka huu 2025 inasema “Kura yako haki yako,jitokeze kupiga kura”