Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
11 October 2025, 11:08 am

ACT-Wazalendo kupitia Mgombea Udiwani wa Kata ya Mbasa amesema Mbasa sio sehemu ya kushindwa kupitika
Na Katalina Liombechi
Mgombea udiwani wa Kata ya Mbasa kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Goodluck Msowoya, amezindua rasmi kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wakazi mbalimbali wa kata hiyo, wanachama wa chama pamoja na viongozi wa ACT-Wazalendo katika ngazi za kata na wilaya.
Akihutubia wakazi wa Mbasa wakati wa uzinduzi huo Oktoba 10,2025 Msowoya amesema kuwa iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Diwani wa kata hiyo, atahakikisha anatekeleza kwa vitendo vipaumbele vyake sambamba na Ilani ya ACT-Wazalendo.
Miongoni mwa vipaumbele alivyoainisha ni pamoja na Kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya kata,Kujenga ofisi ya kisasa ya kata kwa ajili ya kutoa huduma kwa ufanisi,Maboresho katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuongeza miundombinu ya shule na mazingira ya kujifunzia,Kufanikisha upimaji wa ardhi ili wananchi wawe na hati halali za umiliki,Kutenga na kuandaa eneo rasmi la maziko na Kujenga soko la kisasa kwa ajili ya kukuza uchumi wa wananchi.

Vipaumbele vingine ni pamoja ni Kuboresha viwanja vya michezo kwa ajili ya vijana na kukuza vipaji,Kuwezesha mikopo kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,
Kuboreshwa kwa huduma ya maji safi na salama na Kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa uwazi na uwajibikaji.
Chama cha ACT-Wazalendo kupitia kwa Katibu wa chama hicho Wilaya ya Kilombero Bwana Utoto na kusema chama hicho kimeahidi kumpa usaidizi wa karibu mgombea huyo ili kuhakikisha anafanikisha kampeni zake kwa mafanikio na kwa kuzingatia maadili ya kisiasa.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 ambapo wananchi wa Kata ya Mbasa watakuwa na nafasi ya kumchagua kiongozi atakayewakilisha maslahi yao ndani ya baraza la madiwani.