Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
1 October 2025, 7:41 pm

Mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri ya Mlimba kwa gharama ya shilingi bilioni 6, huku kiasi kingine kikitekelezwa katika Wilaya mbili za Zanzibar
Na Katalina Liombechi/Kuruthumu Mkata
Kikao cha siku tatu cha uthibitishaji wa ripoti za tathmini ya mradi wa maboresho mifumo ya chakula, matumizi ya ardhi na urejeshaji wa mazingira (FOLUR)kimeanza leo katika mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau kutoka kongani ya Kilombero pamoja na visiwani Zanzibar, kikilenga kupitia kwa pamoja ripoti za tathmini kabla ya utekelezaji kamili wa mradi huo wenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 18.
Waratibu wa mradi huo kutoka Halmashauri ya Mlimba Joseph Mgana na Miza Khamis upande wa Zanzibar wamesema kikao hicho ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa ripoti zilizotolewa zinazingatia hali halisi ya mazingira ya utekelezaji, pamoja na kutoa fursa kwa wadau kutoa maoni na mapendekezo ya maboresho kabla ya hatua zinazofuata.

Wanjara Mgahywa Mratibu mkuu Mtekelezaji Mradi huo Kitaifa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii amesema katika kikao hicho wataalam na wadau watatoa michango kwenye tahmini na tafiti mbalimbali yanayohusu majukumu ya mradi ambayo yametekelezwa kwa mwaka jana katika maeneo yote ya mradi Mlimba katika Wilaya ya Kilombero na Zanzibar.

Sauti ya Wanjara Mgahywa
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Abrahamu Mwaikwila akifungua kikao hicho akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amesema kikao hicho ni cha makusudi kufanyika kwa wadau sahihi ambapo amewataka kujadiliana kwa kina kuainisha changamoto na namna ya kwenda kutekeleza Mradi wa FOLUR kwa Ufasaha.

Lengo kuu la mradi huo wa Miaka Mitano ni kuimarisha usalama wa chakula, kulinda mazingira, na kuhakikisha matumizi endelevu ya ardhi kwa manufaa ya jamii za sasa na vizazi vijavyo.