Pambazuko FM Radio

DC Kyobya ahamasisha amani kuelekea uchaguzi

11 September 2025, 7:14 pm

Picha ya waandishi wa habari Kilombero na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Mt. Fransisko Ifakara (Picha na Kuruthumu Mkata)

‘Tuendelee kuhamasishana kushiriki kampeni za uchaguzi bila kusababisha taharuki wala kuvuruga amani’

Na Katalina Liombechi

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ameendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na Waandishi wa Habari pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Fransisko Ifakara Ofisini kwake ambapo pamoja na mambo mengine Mh.Kyobya amesema uchaguzi ni sehemu ya demokrasia na unapaswa kuendeshwa kwa heshima, mshikamano na kuzingatia sheria na maelekezo yaliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na vyombo vya dola.

Picha ya Wakili Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao kuendesha kampeni kwa hoja badala ya matusi au vitendo vingine vinavyoweza kuvunja amani na utulivu uliopo kwasasa.

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuanzisha vurugu au kusababisha uvunjifu wa amani katika kipindi hiki muhimu kwa Taifa.