Pambazuko FM Radio

Asenga, Rwakatare waongoza kura za maoni CCM Kilombero

5 August 2025, 7:34 pm

Picha ya Kellenrose Rwakatare(Picha kwa hisani ya Denis Ngalyoma)

Matokeo ya kura za maoni ndani ya CCM ni baada ya kurudi kwa majina ya wagombea na kupitishwa kutambulishwa na Chama kwa wajumbe kwa siku nne na Agosti 5 2025 kupigiwa kura.

Na Katalina Liombechi

Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kilombero Gervas Ndaki amemtaja Abubakar Asenga kuwa mtia nia wa Ubunge  aliyeongoza kwa kupata kura 5033 za maoni kati ya watia nia 8 waliokuwa kwenye mchakato wa huo.

Katibu huyo ameyasema hayo wakati akitangaza matokeo hayo hii leo Agosti 5,2025 mbele ya Waandishi wa Habari,baadhi ya Watia nia wa Ubunge na Udiwani na Viongozi wa Sekretarieti ya CCM Kilombero ambapo amesema wengine waliofuatia katika kura hizo ni Issa Vitus Lipagila aliyepeta kura 807,Abdulla Zulu  Lyana 280,Aloyce Tendewa 340,Denis Bandisa 164 na Salim Mfungahema ambaye amepata kura 53.

Wengine ni Christina Dominic Kulunge aliyepata kura 35 pamoja na Lulu Utoto kura 16.

Picha ya Gervas Ndaki Katibu CCM Kilombero(Picha na Kuruthumu Mkata)

Akizungumza mara baada ya kutangazwa matokeo hayo ndugu Abubakar Asenga ameelezea kupita katika zoezi hilo mchakato huo licha ya kukiri ushindani mkubwa huku akiomba ushirikiano kwa hatua zinazofuata.

Mmoja wa watia nia wengine Christina Dominic Kulunge ameelezea imani yake kwa chama chake huku akitoa wito wa kuendelea kushirika kukijenga chama cha Mapinduzi.

Aidha katika upande wa Jimbo la Mlimba aliyeongoza ni Kellenrose Rwakatare kwa kupata kura  3803 na kufuatiwa na Acley Mhenga aliyepata kura 998.

Kwa mujibu wa katibu huyo matokeo hayo ni baada ya zoezi la kura za maoni lililofanyika Agosti 4,2025 na kwamba hatua inayofuata ni kuelekea mapendekezo na vikao mbalimbali.