Pambazuko FM Radio

Meno sita ya tembo yakamatwa Ulanga

17 July 2025, 7:03 pm

Picha ya RPC Alex Mkama akiwa ameshika meno ya tembo (Picha na Kuruthumu Mkata)

Upelelezi zaidi wa kisayansi unaendelea kuhusiana na utambuzi vinasaba vya wanyama hawa maeneo ambayo wanyama wamepatikana

Na Katalina Liombechi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na maofisa wa wanyamapori wilaya ya Ulanga limefanikiwa kuwakamata watu wawili wakazi wa kijiji cha Isongo wakiwa na meno 6 ya Tembo.

Watuhumiwa hao ni Televaeri Paranjo 47 mkazi wa kijiji cha Isongo na Freddy Maxmilian Magumba 42 mkazi wa kijiji cha Isongo wamekamatwa julai 14,2025 majira ya asubuhi katika kitongoji cha korowa kijiji na kata ya Isongo Wilaya ya ulanga wakiwa pembeni mwa barabara ya mahenge mwaya.

Kwa mujibu wa kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama akizungumza na waandishi wa habari hii leo Julai 17,2025 akiwa Ifarara Wilayani Kilombero amesema   kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni baada ya taarifa fiche zilizotolewa na wananchi walio wema wanaoishi pembezoni mwa hifadhi huku wakiomba ushirikiano zaidi  kutoka kwa wananchi kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kinyume cha sheria.

Picha ya RPC Mkama(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya RPC Mkama

Aidha ametoa wito kwa wananchi hasa wanaoishi jirani na maeneo ya Hifadhi kuendelea kutoa ushirikiano wa vitendo vya uhalifu wa namna hiyo,huku akieleza kuwa wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo na kwamba upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.