Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
2 July 2025, 9:39 pm

Tuna wanachama watatu wameshindwa kurejesha fomu pengine kutokana na sababu mbalimbali ambazo siwezi kuzijua
Na Katalina Liombechi
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kilombero, Gervas Ndaki, ametaja jumla ya wanachama 36 wa chama hicho waliokuwa wamechukua fomu za kugombea ubunge katika majimbo ya Kilombero na Mlimba kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Octoba mwaka huu 2025.
Hata hivyo, kati ya idadi hiyo, ni wagombea 33 pekee ndio waliorejesha fomu zao kwa mujibu wa taratibu za chama, huku watatu wakishindwa kurejesha ndani ya muda uliopangwa.
Ndaki amesema zoezi hilo la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ambalo limekwenda kwa siku 5 kuanzia Juni 28-July 2 2025 limefanyika kwa utulivu na kuzingatia kanuni za chama na sasa hatua inayofuata ni mchakato wa mchujo kupitia vikao vya ngazi mbalimbali vya chama.
Ameeleza kuwa wanachama waliorejesha katika jimbo la Kilombero 19 na Mlimba 14 na kwamba katika idadi hiyo wanawake wawili waliojitokeza kuchukua fomu Mlimba na Kilombero wawili.
Aidha ameelezea mwitikio wa vijana umekuwa mkubwa ambapo katika jimbo la kilombero 9 na Mlimba 7.
Ameongeza kuwa chama kinajivunia mwitikio mkubwa wa wanachama waliokuwa tayari kuomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge, jambo linaloonesha afya ya demokrasia ndani ya CCM.