Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
6 May 2025, 3:32 pm
Na Katalina Liombechi

Mamba mmoja ameuwawa leo asubuhi baada ya kuonekana katika makazi ya watu katika Mtaa wa Jongo, Kata ya Viwanjasitini, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Aikani Kikoti,Leopord Chogo na Grace Maganga wamesema mamba huyo alianza kuonekana majira ya saa 12:00 alfajiri hii leo Mei 6, 2025 katika banda la mifugo la mkazi mmoja wa eneo hilo tukio ambalo liliibua taharuki miongoni mwa wakazi, na baadhi yao walilazimika kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kujilinda, hatua iliyosababisha kuuawa kwa mnyama huyo hatari huku wakielezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya mamba yamekuwa ya kawaida katika maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Jongo, Emmanuel Lusoli, kwa kushirikiana na Mouson Chiwalila kutoka mtaa jirani wa Kilosa, pamoja na Diwani wa Kata hiyo, Mheshimiwa Erick Kulita, na Mtendaji wa Kata ya Viwanjasitini Bi Hawa Ndachuwa, wakiwa katika eneo la tukio walithibitisha kupokea taarifa hizo na kuchukua hatua za haraka.
Viongozi hao wameeleza kuwa mara baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio na kuwasiliana na Watu wa Maliasili na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi na kutoa tahadhari kwa wakazi kuhusu uwepo wa wanyama wakali hasa kipindi hiki cha mvua kinachosababisha baadhi ya wanyama kuvuka mipaka yao ya kawaida.

Afisa Wanyamapori katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Goodluck Mallya amefika katika eneo hilo kutoa Nyara za Serikali na kusaidia kuiteketeza nyama hiyo ambapo amekiri matukio ya Mamba katika mto huo sio mara ya kwanza kuripotiwa hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari kutofika maeneo ya mto na kutokaribia madimbwi hasa wakati huu masika.

Emmanuel Pius Mwinuka ameshuhudia mamba kwa mwaka Jana amewahi kumjeruhi Mtoto wa Dada yake huku akitoa wito kwa Wazazi wengine kuwa Makini na watoto kutowaruhusu kwenda Mtoni ili kuzuia hatari inayoweza kujitokeza.

Tukio hili limeibua mjadala kuhusu usalama wa binadamu na mifugo karibu na maeneo ya mito na vyanzo vya maji, ambapo wananchi wamehimizwa kuwa waangalifu na kutoa taarifa haraka pindi wanapoona viumbe hatari katika makazi yao.