Ulanga: Shule ya msingi Kivukoni yaendelea kufungwa kutokana na mafuriko
8 April 2024, 6:02 pm
“Kama maji yatakauka kabla ya April 15 mwaka huu shule ifunguliwe na kama hayatakauka shule isifunguliwe” Ni maagizo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Ulanga Saida Mahugu.
Na Elias Maganga
Wakati shule zote zikifunguliwa baada ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka, shule ya msingi Kivukoni iliyopo kata ya Minepa katika halmashauri ya wilaya ya Ulanga imeendelea kufungwa kutokana na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni.
Shule hiyo imezingirwa na maji ya mafuriko katika kipindi cha wiki moja iliyopita ambapo yalianza kuingia hapo kidogokidogo hadi Ijumaa ya April 5 mwaka huu alipofika Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Saida Mahugu kujionea hali ilivyo.
Akizungumza na Pambazuko fm, Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ya Kivukoni Vutendile God amesema baada ya Mkurugenzi kufika ametoa maagizo ya shule hiyo kutofunguliwa hadi pale maji yatakapokauka.
Mwalimu Vutendile amesema kwa mujibu wa Mkurugezi, kama maji yatakauka kabla ya April 15 mwaka huu shule ifunguliwwe na kama hayatakauka shule isifunguliwe.
Tangu kuanza kwa mvua za masika katika Bonde la Kilombero linalojumuisha wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi zimeleta athari za mafuriko ambayo yamesababisha baadhi ya watu kukosa makazi, vifo, kuharibika kwa miundombinu ya barabara na reli, baadhi ya wakulima mazao yao kusombwa na maji mashambani.