Dkt. Biteko aipongeza Tanesco kurejesha umeme
2 April 2024, 3:43 pm
“Hakuna mgao wala upungufu wa umeme kwa sasa hiki kilichotokea ni hitilafu kwenye mitambo ya kuzalisha umeme” Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko
Na Elias Maganga
Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amelipongeza shirika la umeme Tanzania {Tanesco} kwa juhudi walizozifanya kuhakikisha umeme unarejea kutokana na hitilafu ya mitambo iliyojitokeza kuanzia majira ya saa nane usiku wa marchi 31 kuamkia april mosi mwaka huu.
Dkt Biteko ametoa pongezi hizo baada ya kufanya ziara ya dharula katika Bwawa la kufua umeme Kidatu April mosi mwaka huu ili kujionea kile kilichosababisha umeme kukatika ambapo amesema hitilafu hiyo imetokana na mvua zilizonyesha marchi 31 mwaka huu na kupelekea mikoa kadhaa kuathirika kwa kukosekana kwa nishati hiyo.
Aidha Dkt Biteko amewatoa hofu wananchi baada ya kurejea kwa huduma ya umeme na kusema kuwa hakuna mgao wala upungufu wa umeme kwa sasa .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya kilombero wakili Dunstan Kyobya ambaye amemuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amewataka watu wanaoishi mabondeni kuhama mara moja,huku akielezea baadhi ya maeneo yaliyoathirika na maji ndani ya mkoa wa morogoro