Sweden yatoa shilingi bilioni 10 utunzaji mazingira
4 June 2023, 4:39 pm
Mradi wa SUSTAIN –ECO utasaidia kuhamasisha shughuli za maendeleo ambazo ni rafiki kwa mazingira ikiwa ni pamoja na kilimo cha kakao, miwa, mpunga, kilimo cha miti na shughuli zingine zinazoendeleza uhifadhi
Na Katalina Liombechi
Mradi wa SUSTAIN-ECO unakwenda kutatua changamoto za shughuli za kibinadamu zinazoharibu bionuai kwa kuchochea utunzaji mifumo ikolojia kwa maendeleo endelevu katika Bonde la Kilombero.
Hayo yamesemwa na meneja wa taasisi inayojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori Afrika AWF Clarence Msafiri na mfuatiliaji wa miradi kutoka shirika la Umoja wa Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira IUCN Calvin Meta katika uzinduzi wa mradi huo awamu ya pili utakaotekelezwa kwa miaka mitatu.
Wamesema mradi huo umekuja mara baada ya kuona changamoto za uharibifu wa mazingira unaotokana na kufanya shughuli za kibinadamu zisizozingatia utunzaji wa mazingira hivyo kutokana na mbinu mpya,teknolojia mpya na mikakati ambayo itatumika katika utekelezaji wa mradi huo itasaidia kuacha mifumo ya ikolojia kubaki katika hali nzuri.
Wamesema kupitia mradi wa SUSTAIN –ECO utasaidia kuhamasisha shughuli za maendeleo ambazo ni rafiki kwa mazingira ikiwa ni pamoja na kilimo cha kakao, miwa, mpunga, kilimo cha miti na shughuli zingine zinazoendeleza uhifadhi.
Wamesema kupitia shughuli hizo wakulima watazalisha kwa tija wakati huo wanahifadhi mazingira.
Mwakilishi kutoka ubalozi wa Sweden hapa Tanzania Brasio Msugu amesema katika mradi huo ubalozi wa serikali ya SWEDEN umechangia kiasi cha Shilingi Bil 10 itakayosaidia kuendeleza shughuli zote za uhifadhi kwa kushirikiana na wadau.
Akizungumza wakati akizindua mradi huo, mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya ameishukuru serikali ya Sweden kwa kuchangia fedha hizo huku akisisitiza ili mradi huo uweze kufanikiwa amewataka wadau wanaotekeleza kushirikisha wananchi kupitia madiwani, viongozi wa serikali pamoja na wadau wengine wa uhifadhi.
Mmoja wa wakulima wa zao la kakao Calister Ngasakwa kutoka kijiji cha Igima halmashauri Mlimba amesema katika mradi huo wanashiriki kutokana na kilimo hicho ambacho kinawanufaisha kiuchumi na kuendelea kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Mradi huo wa SUSTAIN-ECO awamu ya pili unatekelezwa ndani ya muda wa miaka 3 katika halmashauri za Mji wa Ifakara, Mlimba na wilaya ya Kilosa ambapo watekelezaji ni Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika AWF, Shirika la Umoja wa Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira IUCN kwa kushirikiana na Wadau wengine wa uhifadhi wa mazingira huku wafadhili wakiwa ni ubalozi wa serikali ya SWEDEN nchini Tanzania.