Vyama vya ushirika Ifakara vyalia kucheleweshwa kwa mikopo, kutozwa riba kubwa
1 June 2023, 2:33 pm
Na Elias Maganga
Viongozi wa vyama vya ushirika na SACCOS katika halmashauri ya mji wa Ifakara wamemweleza mkuu wa wilaya ya Kilombero changamoto zanazowakabili ikiwa ni pamoja na wavuvi walioomba soko la Kivukoni, na kumiliki mabwawa ya asili bila mafanikio pamoja na mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kutozingatia muda na kutozwa riba kubwa.
Changamoto hizo zimetolewa na mwenyekiti wa kongamano la vyama vya ushirika Bakari Mkangamo kwenye kongamano la vyama vya vya ushirika halmashauri ya mji wa Ifakara liliofanyika kwa lengo la Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstun Kyobya kujitambulisha kwa vyama hivyo,
Akiwasilisha risala kwa mgeni rasmi, Afisa Ushirika wa halmashauri ya mji wa Ifakara Bwana Issa Kilua ameelezea hali ya vyama vya ushirika katika halmashauri hiyo kuwa hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu, jumla vyama vya ushirika 36, ambapo 12 kati ya hivyo ni vyama vya akiba na mikopo, vyama vya mazao na masoko 20, vyama vya ushirika vya uvuvi 3, chama kikuu kimoja na chama cha mradi wa pamoja kimoja, vyote hivyo vikiwa na jumla ya wanachama 10,572.
Aidha Bwana Kilua amesema hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu serikali imewezesha vyama vya ushirika kuwadhamini katika taasisi mbalimbali za kifedha na kuweza kukopa zaidi ya bilioni 14.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya akijibu changamoto zilizowasilishwa na vyama vya ushirika ,amesema wavuvi wajengewe mabwawa ya kisasa na atazungumza na TAWA kuhusu soko la kivukoni na watajibiwa ndani ya muda mfupi
Pia mkuu huyo wa wilaya akazungumzia changamoto ya mikopo kwa vyama vya ushirika
Aidha ameziagiza AMCOS zote kuajiri wataalam kutokana na changamoto walizonazo ndani ya miezi mitatu toka sasa. Amemwagiza pia Afisa Ushirika kiundwe chombo kitakachosimamia vyama vya ushirika vyote ndani ya wilaya ya Kilombero huku akisisitiza mikutano ya vyama hivyo vifanyike mara mbili kwa mwaka.
Kongamano hilo liliobeba kauli mbiu isemayo “Ushirika ni Biashara, Ushirika kwa Maendeleo Endelevu” lilitanguliwa na maandamano yaliyopokelewa na mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya