Dhana ya Afya Moja katika kutatua changamoto za kiafya
16 May 2023, 7:28 pm
Udhibiti wa magonjwa mbalimbali hauwezi kupatikana kwa kutumia wataalam wa sekta husika pekee hivyo kwa kutumia dhana ya Afya Moja itasaidia kupata suluhu ya afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira.
Na Katalina Liombechi
Wataalam wa sekta mbalimbali katika bonde la Kilombero wametakiwa kutumia dhana ya Afya Moja katika kushirikiana na kutatua changamoto za kiafya zinazojitokeza katika jamii.
Hayo yamesemwa na mtaalam wa Afya ya Mifugo na Afya Shirikishi kutoka Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro Prof. Robinson Mdegela katika warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Uhifadhi wa Wanyamapori AWF kwa kushirikiana na IUCN iliyofanyika katika ukumbi wa TTCIH Ifakara.
Prof. Mdegela amesema udhibiti wa magonjwa mbalimbali hauwezi kupatikana kwa kutumia wataalam wa sekta husika pekee hivyo kwa kutumia dhana ya Afya Moja itasaidia kupata suluhu ya afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira.
Amesema katika jamii kumekuwa na magonjwa ambayo yanatokea kutokana na mwingiliano kati ya binadamu na makazi ya wanyamapori huku akitolea mfano ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambacho kinagharimu maisha ya watu na uchumi wa taifa.
Mtaalam wa Afya ya Mifugo na Afya Shirikishi kutoka Chuo kikuu cha Kilimo SUA Prof Robnson Mdegela{Picha na Katalina Liombechi}
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amesema Afya Moja iende sambamba na uhifadhi wa mazingira ili kuzuia athari za magonjwa yanayotokana na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Amesema hatawavumilia watu wanaofanya uharibifu katika Bonde la Mto Kilombero kwani Mto huo unachangia asilimia 65 ya maji yake kwenda katika Mradi Mkubwa wa Uzalishaji Umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere huku akisisitiza Upandaji wa Miti na kutoa elimu ya Uhifadhi wa Mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya{Picha na Kataliana Liombechi}
Kwa upande wake Meneja wa Taasisi inayojihusisha na Uhifadhi wa Wanyamapori (AWF) Clarence Msafiri amesema lengo la kukutanisha jopo la wataalam kutoka katika maeneo hayo ni kuwapatia uelewa juu ya dhana ya Afya moja na namna itakavyosaidia kutatua changamoto za kiafya kwa Binadamu,Wanyama na Mazingira kwa ujumla.
Meneja wa Taasisi inayojihusisha na Uhifadhi wa Wanyamapori (AWF) Clarence Msafiri {Picha na Katalina Liombechi}
Baadhi ya Wataalam waliopata Elimu hiyo ya Afya Moja Afisa Maliasili Wilaya ya Malinyi Asma Chamshara,Afisa Uvuvi kutoka Wilaya ya Ulanga Daniel Bwanaheri na Afisa Mazingira Justine Bundu wamesema wataenda kushirikiana katika kutatua changamoto za kiafya katika jamii kwa kutoa Elimu na kushirikisha Mawazo kupata suluhu.
Ikumbukwe kuwa Elimu hiyo ya Dhana ya Afya Moja imeanza kutolewa kuanzia Ngazi ya Taifa,Mkoa na Eneo la Bonde la Kilombero ambapo imetolewa kwa Wataalam wa Sekta mbalimbali kutoka katika Halmashauri za Wilaya Malinyi,Ulanga Mlimba na Mji wa Ifakara,Mafunzo ambayo yameandaliwa na Taasisi ya Uhifadhi wa Wanyamapori AWF kwa Kushirikiana na IUCN na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa TTCIH Ifakara.