mafuriko ya haribu miundombinu ya barabara na makazi ya watu Ifakara
27 April 2023, 11:44 pm
Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro zimesababisha mafuriko na athari katika baadhi ya maeneo ikiwemo kitongoji cha Kwa shungu, kata ya Mbasa na Lumemo kata ya Lumemo halmashauri ya mji wa Ifakara.
Na; Isidory Mtunda
Kata sita za halmashauri ya mji wa Ifakara wilaya Kilombero mkoani Morogoro zimeathiriwa na mafuriko kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili Aprili 23, 2023.
Wakizungumza na Pambazuko fm Aprili 23, 2023 baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Kwa shungu, kata ya Mbasa halmashauri ya mji wa Ifakara, Imelda Malema, Hilda Chikopa na Jenifa Makayula wamesema mafuriko hayo yamesomba Unga, mchele Maharagwe na Magodoro pia yameribu mazao.
Waathirika hao wameomba uongozi wa halmashauri ya mji wa Ifakara, hususan kama ya maafa kupeleka msaada wa haraka wa chakula na mahitaji mengine muhimu katika kaya zilizokumbwa na mafuriko hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji cha kwa shungu bwana Shabani Msowale amesema kuwa robo tatu ya kitongoji hicho kimeathiriwa na mafuriko hayo na ameoimba serikali ya wilaya hiyo kupeleka wataalam haraka kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari zilizotokana na mafuriko hayo.
Kwa upande wake mratibu wa maafa halmashauri ya mji wa Ifakara Brigita Haule, amesema madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo ni pamoja na, uharibifu wa miundo mbinu ya barabara na makazi ya watu.
Bi Haule amesema mafuriko hayo yameathiri barabara ya Ifakara kidatu, nyumba nane zilizopo kata ya Lumemo , shule ya msingi Maendeleo na shule ya sekondari kwa Shungu zenyewe zimezingirwa na maji.
Bi Haule ameishauri jamii kuchukua tahadhari za kiafya kwa kunywa maji yaliyochemshwa, kunawa mikono kwa sabuni na kula vyakula vya moto ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindu pindu.
Mratibu huyo ametaja maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo kuwa ni kata za; Mbasa, Viwanja sitini, Mwaya, Kidatu Lumemo na Kata ya Ifakara.