Serikali ya Kijiji yadaiwa kupora ardhi.
15 March 2023, 11:36 am
Na Isdory Mtunda
Miongoni wa changamoto zinazowakumba baadhi ya wananchi wa Vijiji vya Igota na Magereza ,Wilayani Ulanga Mkoani Morogoro ,ni kuporwa ardhi na Serikali ya Kijiji.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wananchi wa Vijiji hivyo katika mkutano uliowakutanisha wananchi pamoja na Kituo cha msaada wa kisheria Morogoro wakati wakitoa elimu kwa jamii kuhusu Talaka, Mirathi, Wosia, Ukatili na Migogoro ya ardhi.
Katika mkutano huo bi Olga Mtitu mkazi wa Igota ametoa kero yake dhidi ya serikali ya kijiji cha Igota , ambapo anadai kunyang’anywa eneo lake lenye ukubwa wa heka kumi, eneo ambalo lilikuwa pori wakasafisha yeye na mume wake.
Marcus Milanzi mtendaji wa kijijji cha Igota, amesema taarifa ya mama huyo ipo ofisini na kwamba mchakato unafanyika ili mama huyo arudishiwe eneo lake baada ya msimu huu wa kilimo kuisha
Afisa uhusiano na utawala wa Kituo cha msaada wa kisheria Morogoro Bwana Peter Kimath, amesema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea uelewa wananchi na mabaraza ya kata juu ya Talaka, Mirath, wosia, ukatili na masuala ya ardhi.
Katika mkutano wa kijiji cha Igota kata ya Lupiro jumla ya kesi saba zimeibuliwa , ambazo kituo cha msaada wa kisheria Morogoro watazifuatilia na kutoa msaada wa kisheria wakisaidiana na wasaidizi wa kisheria kijijini hapo.