Wazazi wasiowapeleka watoto shule kukiona
31 January 2023, 8:33 am
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Dunstan Kyobya amewaagiza maafisa Watendaji wa Vijiji na Kata kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni.
Bwana kyobya ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa umma,viongozi wa dini pamoja na viongozi kutoka sekta binafsi kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Kata ya Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Amesema tayari shule zimeshafunguliwa na baadhi ya watoto hawajaripoti shuleni kwa madarasa ya awali,la kwanza na kidato cha kwanza na mwisho wa kuripoti ni januari 31 mwaka huu baada ya hapo watendaji wachukue hatua kwa wazazi wa watoto ambao watakuwa hawajaripoti.
Aidha amewataka walimu wakuu na wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi hata kama hawana sare,viatu huku wazazi wakiendelea kujipanga kukamilisha mahitaji ya mtoto.
Tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero na Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan , hiki ni kikao chake cha kwanza kukifanya huku lengo likiwa ni kujitambulisha na kueleza mikakati atakayoanza nayo.