Uhalifu Wapungua 75%,Wananchi waondolewa Hofu
18 May 2021, 5:36 am
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mangwale Kata ya viwanja sitini katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero wameeleza wasiwasi wao juu ya vitendo vya kiuhalifu vinavyotokea kwenye mtaa huo.
Wakizungumza na pambazukofm baadhi ya wakazi hao akiwemo Joyce Kaonja na Peter Kinjara wamesema vitendo vya uhalifu hususani wizi umekithiri katika mtaa huo ambapo wamedai kuwa wizi huo umefanyika hasa katika kipindi cha masika.
Wakazi hao wa mtaa wa mangwale wamesema kuwa vitendo vya wizi vinarudisha nyuma maendeleo ya watu kwani mpaka sasa wamedai kuwa ni watu wengi waliolalamika kuibiwa.
Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mangwale Bwana Henrick Ngulukila amekiri kuwepo kwa wizi katika mtaa huo na ameongeza kuwa jitahada za viongozi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuwakamata baadhi ya wahalifu na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Bwana Ngulukila amesema kufuatia kukamatwa na kufungwa kwa wahalifu hao ,vitendo vya wizi vimepungua kwa asilimia 75 huku jitihada za kuendelea kuwasaka wezi zikiendelea.