Boma Hai FM
Boma Hai FM
19 March 2026, 5:22 pm

Juhudi za kulinda vyanzo vya maji zimeendelea kupewa kipaumbele wilayani Hai, huku viongozi wakisisitiza ushirikishwaji wa wananchi ili kudumisha upatikanaji wa maji safi na salama,Mafanikio ya Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe yamepongezwa kwa kung’ara kitaifa, wakati hatua za kudhibiti uharibifu wa miundombinu pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii zikiendelea kuimarishwa.
Na Elizabeth Mafie
Mkuu wa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Hassani Bomboko amezitaka bodi za maji wilaya ya Hai kuendelea kulinda na kutunza, vyanzo vya maji kwa kushirikisha wananchi ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaendelea kupatikana bila vikwazo.

Bomboko ametoa kauli hiyo Machi 18, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji kiwilaya, yaliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira (RUWASSA) wilaya ya Hai.

Bomboko amesema ushirikishwaji wa wananchi ni muhimu katika kulinda vyanzo vya maji, na kuonya kuwa Iwapo zipo shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye maeneo ya vyanzo hivyo zinapaswa kusitishwa mara moja ili kuepusha uharibifu.
Katika hatua nyingine, Bomboko ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira(RUWASSA) pamoja na bodi za maji kwa juhudi zao za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwani Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe imekuwa mfano bora, akibainisha kuwa imefanikiwa kushinda tuzo ya bodi bora mkoani Kilimanjaro kati ya bodi 35, pamoja na kutunukiwa tuzo ya kitaifa kwa utoaji wa huduma bora.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka, amezipongeza bodi za maji kwa kuhakikisha huduma inapatikana wakati wote licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Hai Wanguba Maganda, amezitaka bodi hizo kutoa elimu kwa wananchi wanaoharibu miundombinu ya maji, ikiwemo kukata mabomba, na kusisitiza kuwepo kwa adhabu kali kwa waharibifu.
Akizungumzia uzinduzi huo,kaimu Meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira( RUWASSA )wilaya ya Hai, Mhandisi Benedcti Daniel, amesema miti 100 imepandwa katika chanzo cha maji Kikafu Soka kama sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kwamba elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Hata hivyo meneja wa Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe Mhandisi Anord Mbaruku, amesema mafanikio yao yametokana na utendaji mzuri na utoaji bora wa huduma, huku akiahidi kuendelea kuboresha huduma na kuwakumbusha wananchi kulipa ankara za maji kwa wakati.
Wiki ya maji huadhimishwa kote duniani kila ifikapo Machi 16 na kilele chake ni Machi 22 ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Morogoro yakiongozwa na kauli mbiu isemayo”Rasilimali za maji na usawa wa kijinsia”
