Boma Hai FM
Boma Hai FM
18 March 2026, 10:20 am

Miti zaidi ya 200 imepandwa katika shule ya sekondari Kwamkombozi katika kata ya Masama Kusini Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali hasa shule na kampeni ya ”Soma na Mti”
Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Wanafunzi wa shule ya sekondari Kwamkombozi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutunza mazingira kwa kulinda na kuitunza miti iliyopandwa katika maeneo yanayoizunguka shule hiyo.
Wito huo umetolewa Machi 17, 2026 shuleni hapo na Mhifadhi Misitu (TFS) wilaya ya Hai Marsia Aloyce Nguma wakati wa zoezi la upandaji miti ambapo zaidi ya miti miambili Imepandwa katika shule hiyo ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la upandaji miti katika shule hiyo ambapo kwa siku ya leo ni awamu ya tatu kuanzia kuanzishwa kwa kampeni ya “Soma na Mti”
Marsia mesema wanaendelea na zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali ili kulinda ardhi dhidi ya mmomonyoko, pamoja na kurudisha thamani ya ardhi na mazingira katika hali yake ya asili.
Pia ametoa wito kwa wanafunzi na jamii ya watu wanaozunguka katika maeneo ambayo miti imepandwa kuhakikisha miti hiyo inalindwa kwa ukaribu na kuhakikisha inakua vizuri bila kufa hata Mti Mmoja.

Nae afisa misitu wilaya ya Hai John Katikiro amesema kupanda miti ni utamaduni mzuri kwa sababu miti inafaida nyingi katika maisha yetu ya kila siku, akihimiza kuwa kila mwanafunzi anapaswa kulinda miti hiyo iliyopandwa katika shule hiyo kwa kuwa matarajio ni makubwa katika kukuza na kulinda miti katika maeneo ya shule hiyo.
Mkuu wa shule hiyo mwalimu Acheni Kigava ameishukuru serikali kwa kuwapa miti miambili ambayo imepandwa katika Shule yake, ameahidi kuitunza miti hiyo ambapo wameweka mikakati ya kila mwanafunzi kutunza Mti wake na kuhakikisha miti hiyo inakua.
