Boma Hai FM
Boma Hai FM
13 March 2026, 12:45 am

Wananchi mkoani Kilimanjaro wameshiriki zoezi la Samia Ardhi Kliniki lililoendeshwa kwa wiki nzima mkoani humo, ambapo wamepatiwa elimu kuhusu matumizi bora ya ardhi, viwanja vimepimwa, kurasimishwa na wananchi kukabidhiwa hati miliki
Na Henry Keto, Siha-Kilimanjaro
Wananchi mkoani Kilimanjaro wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la Samia Ardhi Kliniki lililoendeshwa kwa wiki nzima mkoani humo, ambapo mbali na kupatiwa elimu kuhusu matumizi bora ya ardhi, baadhi ya viwanja vimepimwa, kurasimishwa na wananchi kukabidhiwa hati za umiliki
Akizungumza wakati wa kufunga zoezi hilo lililofanyika katika eneo la wazi la Ofisi ya Kata ya Ormelili wilayani Siha, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro, Rehema Mdee, amesema lengo la kliniki hiyo ni kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na kurahisisha upatikanaji wa hati za umiliki kwa wananchi.
Amesema kupitia zoezi hilo wananchi wamepata elimu kuhusu matumizi sahihi ya ardhi, taratibu za upimaji wa viwanja na namna ya kurasimisha maeneo yao ili kumiliki ardhi kisheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, amewahimiza wananchi kutumia fursa ya kliniki hiyo kutatua changamoto za ardhi na kuhakikisha wanapima na kurasimisha maeneo yao ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Wananchi walioshiriki katika kliniki hiyo wamesema mpango huo umewasaidia kupata ufafanuzi wa changamoto mbalimbali za ardhi na baadhi yao kufanikiwa kutatuliwa kero zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.