Boma Hai FM

Timu ya Hai United yaendelea kujinoa kuelekea Ligi ya mabingwa mkoa

11 March 2026, 12:07 pm

Pichani ni wachezaji wa Hai United wakiwa na mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko(aliyevaa kofia)picha na mwandishi wetu.

Maandalizi ya timu ya Hai United kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Mkoa yanaendelea kushika kasi huku kikosi hicho kikikusanyika kambini kwa mazoezi maalum ya kujiimarisha kiufundi na kimwili.

Na mwandishi wetu Hai-Kilimanjaro

Timu ya mpira wa miguu  ya Hai United imeendelea na kambi yake ya maandalizi kuelekea michuano ya ligi ya mabingwa mkoa inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Hai United ambayo inapeperusha bendera ya mkoa wa Kilimanjaro katika michuano hiyo, imeanza rasmi kambi yake ya maandalizi  na hadi kufikia leo jumla ya wachezaji 24 wakiwa tayari wamewasili kambini huku wachezaji wengine wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo jioni ya leo.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu hiyo msemaji wa Hai United Edwine Lamtey, amesema kuwa maandalizi muhimu kwa ajili ya michuano hiyo yamekamilika kwa kiwango kikubwa, na kwa sasa wachezaji wanaendelea kupokea maelekezo muhimu kutoka kwa kocha wa timu.

Lamtey amesema mwalimu wa timu tayari amekabidhiwa kikosi na anaendelea kutoa mazoezi ya kila siku pamoja na mbinu mbalimbali zitakazosaidia timu kufuzu hatua inayofuata.

Sauti ya msemaji wa Hai United Edwin Lamtey

“Mwalimu amekwishakabidhiwa timu na anaendelea kuwapa mazoezi ya kila siku pamoja na maelekezo ya namna bora ya kufuzu na  kiujumla timu yetu imedhamiria kufuzu katika hatua hii muhimu, na tunaamini tuna uwezo wa kutinga hatua inayofuata na kuweka rekodi mpya,” amesema Lamtey.