Boma Hai FM

RC Babu ahimiza usawa wa haki kwa wanawake na wasichana Kilimanjaro

11 March 2026, 11:53 am

Pichani ni baadhi ya wanawake wa mkoa wa Kilimanjaro wakiwa katika maandamano ya amani kuelekea katika viwanja vya shule ya sekondari Mailisita wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro(picha na Salma Mgosso)

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kimkoa katika mkoa wa Kilimanjaro yametumika kuhimiza usawa wa haki na fursa kwa wanawake na wasichana ili kuharakisha maendeleo ya jamii.

Na Salma Mgosso Hai-Kilimanjaro.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050” ni wito wa mabadiliko ya fikra ili kuwawezesha wanawake kupata haki zao na kujikwamua kiuchumi pamoja na kusaidia vizazi vijavyo kufikia maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza  Machi 9, 2026 katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya sekondari Maili Sita wilayani Hai mkoani Kilimanjaro  Babu amesema serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa wanawake na wasichana, hivyo imeendelea kuongeza shule pamoja na vifaa vya kufundishia katika Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba  mkoa huo unajivunia kuona wanawake wengi wakishika nafasi mbalimbali za uongozi kama wakurugenzi, wakuu wa wilaya, mahakimu, maafisa wa polisi, OCD pamoja na wanahabari.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.

Kwa upande wake  mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuwawezesha wanawake kupitia mikopo ya halmashauri na semina mbalimbali, bado kuna changamoto ya baadhi ya wanawake kunyimwa haki ya kurithi ardhi, hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na shughuli za maendeleo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko.

Wanawake waliohudhuria maadhimisho hayo wamesema wanajivunia hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuwawezesha wanawake na wameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na ndoa na mimba za utotoni.

Pichani ni mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu(katikati)pamoja na viongozi wengine akikagua mabanda mbalimbali katika maadhimisho ya siku wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya sekondari Mailisita wilayani Hai mkaoni Kilimanjaro(picha na Salma Mgosso)