Boma Hai FM
Boma Hai FM
6 March 2026, 2:13 pm

Katika kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza kipato cha familia,wananchi hao wameaswa kurejesha mikopo wanayopatiwa na serikali.
Na Oliva Joel
Hai – Kilimanjaro
Imeelezwa kuwa kukosekana kwa uaminifu wa kurejesha mikopo inayotolewa na halmashauri na ile ya mtu mmoja mmoja kwa wakati kunawanyima fursa wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo yenye riba nafuu.
Hayo yamebainishwa Machi 4, 2026 na afisa mahusinao kutoka NMB Bank Alexander Fabian wilaya ya Hai, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano uliofanyika katika ofisi ya kijiji cha Lemira Kati, kata ya Masama Kati wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Amesema benki hiyo imepewa dhamana ya kusimamia utoaji wa mikopo yenye riba ya asilimia saba inayotolewa kupitia mpango unaoungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Fabian amesema ili mjasiriamali aweze kupata mkopo huo anatakiwa kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali, awe na umri wa miaka 18 hadi 75, na asiwe na deni katika taasisi yoyote ya kifedha.

Aidha ameongeza kuwa mwombaji wa mkopo anapaswa kuwa tayari anaendesha biashara kabla ya kuomba mkopo, ili kuonesha kuwa ana uzoefu wa biashara na uwezo wa kurejesha mkopo kwa wakati.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Masama Kati Kandata Kimaro, amesema mikopo inayotolewa na serikali inalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto za maisha.
Amesema changamoto ya baadhi ya mikopo ya asilimia 10 kutorejeshwa kwa wakati inatokana na baadhi ya wanakikundi kukosa uaminifu n kwamba mfumo wa mikopo ya mtu mmoja mmoja unaotolewa kupitia NMB Bank unaweza kusaidia kupunguza changamoto hiyo kwa kuwa kila mkopaji atawajibika kurejesha mkopo wake binafsi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Hai Augustin Mfinanga, amesema ili mjasiriamali apate kitambulisho cha mjasiriamali anatakiwa kujaza fomu inayotolewa na maafisa maendeleo ya jamii katika kata zao kwa gharama ya shilingi elfu ishirini tuu.

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Mary Jimrod Temba na Giliad Kweka wameshukuru kwa elimu waliyoipata, wakisema kuwa mikopo ya riba ya asilimia saba itawasaidia kukuza biashara zao na kuondokana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo kausha damu.