Boma Hai FM

Tutasikiliza kero za wananchi tarafa kwa tarafa-Dc Bomboko

6 March 2026, 1:20 pm

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko (katikati) akiwa katika kikao cha kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi (picha na Salma Mgosso)

Ikiwa zimepita siku kumi na mbili pekee tangu ziara ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba, mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko ameendelea kusikiliza kero za wananchi wa wilaya ya Hai na kuzitatua.

Na Elizabeth Mafie & Salma Mgosso

Hai-Kilimanjaro

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Hassan  Omar Bomboko amesema serikali itaendelea kusikiliza na kutatua kero za wananchi ili kuboresha huduma na maendeleo na kwamba utaratibu huo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi.

Akizungumza katika kikao cha kusikiliza kero za wananchi Machi 5, 2026 katika viwanja vya Ofisi ya mkuu wa wilaya, Bomboko ameainisha baadhi ya kero zilizowasilishwa hapo awali ambazo ni kuhusu huduma za kijamii, miundombinu ya barabara, maji na umeme pamoja malalamiko yanayohusu mikopo, huduma za afya pamoja na migogoro ya ardhi na mirathi iliyowasilishwa na wananchi wakati wa ziara ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt Mwigulu Lameck Nchemba.

Pichani ni wananchi mbalmbali waliofika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Hai kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kero zao (picha na Salma Mgosso)

 Bomboko amebainisha kuwa kutokana na maelekezo ya waziri mkuu ya kushughulikia kero za wananchi na kutokuzoea matatizo yao, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Hai imeendaa utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kila wiki siku ya alhamis ofosini kwake na mara baada ya hapo  atasilikiza kero katika tarafa zote za wilaya ya Hai lengo ikiwa ni kutatua kero hizo kwa wakati .

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko

Katika kikao hicho wananchi walisikilizwa kero zao mojawapo ikiwa ni  mgogoro wa ardhi  katika shule ya msingi Gezaulole ambapo wananchi hao walilalamika kuhusu eneo wakitaka fidia ambapo mkuu wa wilaya ameagiza wananchi hao kulipwa fidia ya viwanja  au wafanyiwe tathimini na wapatiwe fedha na kwamba wapo baadhi wananchi waliingilia eneo la barabara hivyo ni wajibu wao kuondoka pamoja na wale ambao tayari wamepatiwa fidia.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko akitaka wananchi hao wapewe fidia.

Katika hatua nyingine Bomboko amemtaka mkurugenzi wa Rozina Orphan Center Rozmin Njau  kufuata taratibu za kusajili makao ya kuelea watoto yatima kwani malalamiko yake yanatokana na yeye kutofuata utaratibu unaotakiwa.

Pichani ni mwananchi wa wilaya ya Hai Rozlin Njau akiwasilisha kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Hai(picha na Salma Mgosso)

Kwa upande wake, diwani  wa kata ya Bomang’ombe Evod Njau, amesema wananchi wa wilaya ya Hai wameanza kuyaona matunda ya ziara ya waziri mkuu Mwigulu Lameck Nchemba kwani baadhi ya kero zilizokuwa zikiwakabili wananchi zimeanza  kutatuliwa.

Sauti ya diwani kata ya Boman’gombe Evod Njau.

Kwa upande wao wananchi waliotatuliwa kero zao  hususani migogoro ya ardhi katika kikao hicho wamemshukuru mkuu wa wilaya ya Hai kwani kero zao zimetatuliwa kwa wakati  na  wanaamini zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.

Sauti za wananchi wa wilaya ya Hai ambao kero zao zimesikilizwa na kutatuliwa na mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko.

 Hata hivyo Bomboko amemtaka afisa ardhi wilaya ya Hai kumuondoa mara moja mwananchi ambae inadaiwa amelipwa fidia lakini amegoma kuachia eneo  na kwamba maeneo yote ya Halmashauri yapatiwe Hati.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omary Bomboko.