Boma Hai FM

Usajili wa walowezi watajwa chanzo cha upatikanaji wa haki za kijamii

1 March 2026, 12:18 pm

Pichani ni Afisa Uhamiaji wilaya ya Hai SSI Lucy Ikambo Basile (Picha na James Gasindi)

Afisa uhamiaji wilaya ya Hai ametoa wito kwa walowezi wanaoishi katika wilaya ya Hai na maeneo mwngine kujitokeza kusajiliwa kwa hiari ili kukamilisha taratibu za kisheria ili kupata haki stahiki za kuishi kama raia wanaotambulika na hii itasaidia kupatikana kwa haki za kijamii

Na James Gasindi, Hai-Kiliamnjaro

Walowezi wanaoishi katika Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani wametakiwa kujitokeza kwa hiari kujiandikisha na kukamilisha taratibu za kisheria ili kupata vitambulisho na vibali halali vya uhamiaji vitakavyowaruhusu kuendelea kuishi na kufanya shughuli zao nchini kwa mujibu wa sheria.

Wito huo umetolewa na Afisa Uhamiaji Wilaya ya Hai, SSI Lucy Ikambo Basile katika mahojiano maalum na Redio Boma Hai FM 89.3, februari 27,2026 ambapo amesema zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa kila mgeni au mlowezi anayeishi nchini anatambulika rasmi na anapatiwa hadhi stahiki kisheria na kwamba hatua hiyo inalenga kulinda maslahi ya taifa pamoja na haki za muhusika.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ya uhamiaji Tanzania na kanuni zake, mgeni yeyote anayetaka kuishi, kufanya kazi, kuwekeza au kushiriki shughuli za kijamii nchini anatakiwa kuwa na kibali halali cha kuingia na kuishi (residence permit) pamoja na nyaraka nyingine za utambulisho zinazotolewa na mamlaka husika na kwamba kutokuwa na nyaraka hizo ni kosa kisheria na kunaweza kusababisha hatua za kiutawala au kisheria kuchukuliwa dhidi ya muhusika.

Sauti ya Afisa uhamiaji wilaya ya Uhamiaji SSI Lucy Basile akizungumza katika mazungumzo maalumu

Aidha amesema mlowezi aliyesajiliwa rasmi hupata manufaa mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo uwezo wa kufungua akaunti za benki, kuingia mikataba ya kibiashara, kupata huduma za kijamii kwa mujibu wa sheria, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo bila hofu ya kukiuka taratibu za uhamiaji huku usajili huo pia huwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za wageni waliopo nchini kwa ajili ya mipango ya maendeleo na masuala ya kiusalama.

Ameongeza kuwa wilaya ya Hai ni eneo lenye mchanganyiko wa shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji, hali inayovutia watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa kila mlowezi kuhakikisha anakuwa na vibali sahihi vinavyolingana na aina ya shughuli anazofanya.

Katika mahojiano hayo amesisitiza kuwa Idara ya Uhamiaji ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wale wote watakaofika ofisini kwa ajili ya ushauri na kukamilisha taratibu zao na kwamba zipo taratibu za kisheria unaoruhusu mtu aliyeishi nchini bila vibali halali kujisalimisha na kufuata taratibu stahiki bila bughudha, endapo atashirikiana na mamlaka kwa uwazi na uaminifu.