Boma Hai FM
Boma Hai FM
12 February 2026, 5:19 pm

Katika kuwapa motisha wanafunzi wa shule ya sekondari Lemira iliyopo wilayani Hai ,Mkoani Kilimanjaro wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2025 wapewa zawadi.
Na Oliva Joel
Hai- Kilimanjaro
Wazazi na walezi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kushirikiana kwa karibu na walimu wanaowafundisha watoto wao kwa kuwezesha upatikanaji wa mahitaji muhimu yatakayowasaidia wanafunzi kufikia malengo yao ya kielimu.
Wito huo umetolewa februari 11, 2026 na diwani wa kata ya Masama Kati Kandata Kimaro, wakati akizungumza katika kikao cha wazazi kilichofanyika katika shule ya sekondari Lemira.
Kandata ambaye pia ni mzazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, amesema kuwa kukosekana kwa mahitaji muhimu ya mwanafunzi kama vile chakula kunachochea baadhi ya wanafunzi kujiingiza katika vitendo viovu.
Kandata ameeleza kuwa ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanawapatia wanafunzi mahitaji muhimu, ikiwemo kulipia gharama za chakula, pamoja na kununua rim kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ili waweze kufanya majaribio ya mara kwa mara yatakayowawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao.
Hata hivyo, Kandata amewapongeza wanafunzi watatu wa shule hiyo waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2025 kwa kupata daraja la kwanza,ambapo wanafunzi hao ni Caroline Wilson aliyepata divisheni 1.7, Sostenes Lema aliyepata divisheni 1.13 na Tumaini Swai aliyepata divisheni 1.17 kati ya wanafunzi 76 waliofanya mitihani hiyo.
Hata hivyo Katika tukio hilo, mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo ametoa kiasi cha shilingi laki moja kwa wanafunzi hao kama pongezi.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Silvesta Philipo, amewataka wazazi wenye wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kuepuka kuwapa majukumu mengi kupita kiasi wanafunzi hao wawapo nyumbani, akisema hali hiyo inasababisha wanafunzi kushindwa kusoma kwa ufanisi.
Nao baadhi ya wazazi walioshiriki katika mkutano huo akiwemo Gladness Nnko na Moses Lema, wamekubaliana na maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo, ikiwemo kutoa michango muhimu shuleni pamoja na kutoa rim moja kwa kila mwanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ili kuwawezesha kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kufaulu katika mitihani yao ya taifa.