Boma Hai FM
Boma Hai FM
12 February 2026, 4:06 pm

Kutokana na baadhi ya jamii kutowajali ,kuwathamini watu wenye mahitaji maalumu taasisi ya New life Foundition kwa kushirikiana na Tim Tebow Foundation imekusudia kurejesha tabasamu kwa kuwakutanisha kupitia sherehe maalumu.
Na Elizabeth Mafie
Moshi -Kilimanjaro
Jamii imetakiwa kuendelea kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalumu kwa kuwathamini, kuwatambua na kuepuka kuwaficha, ikiwa ni jitihada za kujenga jamii jumuishi yenye upendo, usawa na haki kwa watu wote.
Wito huo unakuja wakati ambapo baadhi ya watu wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za unyanyapaa, ubaguzi na kukosa msaada wa kutosha kutoka kwa jamii inayowazunguka, hali inayochangia kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia na kijamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, baadhi ya walimu wanaohudumia watoto wenye mahitaji maalumu wameeleza kuwa watoto hao hukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo mitazamo hasi kutoka kwa jamii.
Walimu hao wamesema hali hiyo huathiri kisaikolojia watoto hao, ingawa wamesema kwa sasa kuna dalili za muamko chanya unaoendelea kujitokeza, wakisisitiza umuhimu wa juhudi zaidi ili kubadilisha kabisa mtazamo wa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari februari 9,2026 mkurugenzi wa New Life Foundation, Askofu Glorious Shoo, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Tim Tebow Foundation imeandaa tukio maalum lijulikanalo kama Night To Shine, lenye lengo la kuwakutanisha na kuwathamini watu wenye mahitaji maalumu kupitia sherehe maalum itakayowaacha na kumbukumbu ya kipekee katika maisha yao.
Askofu Shoo amesema jumla ya watu 110 wenye mahitaji maalumu wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo, ambapo kila mmoja ataambatana na mshiriki mmoja, huku pia kukiwa na wajitolea 110 kutoka Shirika la New Life Foundation watakaowahudumia washiriki hao kwa siku nzima, kuhakikisha wanaheshimiwa, wanathaminiwa na wanapata huduma bora katika tukio hilo la usiku maalum wa kung’ara.
Amesema Night To Shine ni sehemu ya mapambano ya kubadili mtazamo wa jamii, kuondoa unyanyapaa na kuimarisha kujikubali kwa watu wenye mahitaji maalumu, kwa kuonyesha kuwa nao ni sehemu muhimu ya jamii na wanastahili heshima, upendo na haki sawa na wengine.