Boma Hai FM
Boma Hai FM
5 February 2026, 3:22 pm

Viongozi katika ngazi mbalimbali wameendelea kuhamasisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kushiriana na wananchi kwa kupanda miti sehemu mbalimbali.
Na Oliva Joel
Hai-Kilimanjaro
Wananchi wa kata ya Romu wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro wamehimizwa kupanda miti katika maeneo yanayowazunguka ili kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Romu, Salim Mfoy wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo waliokujitokeza kwa wingi kupanda miti 100 katika eneo la shule ya msingi Tolu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mfoy amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoendelea duniani, wameamua kupanda miti katika eneo hilo la shule ambalo limekumbwa na ukame, kwa lengo la kuboresha mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kata ya Romu Anandumi Kimaro, amesema kuwa miti iliyopandwa katika shule hiyo inapaswa kulindwa na wananchi kwa pamoja, akisisitiza umuhimu wa kuepuka kupitisha mifugo katika eneo hilo ili kuhakikisha miti hiyo inakua.

Naye mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Tolu Joram Welega, amesema kuwa shule imeweka utaratibu wa kila wanafunzi wawili kuwajibika kumwagilia mti mmoja kila siku wanapokuwa shuleni, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi tabia ya kupenda na kutunza mazingira tangu wakiwa wadogo.