Boma Hai FM

Romu, Masama Kusini kuondokana na adha ya maji ya umwagiliaji

5 February 2026, 3:00 pm

Pichani ni Diwani wa kata ya Masama Kusini (kushoto) pamoja na Diwani wa kata ya Romu zilizopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro (Picha Na Henry Keto)

Wananchi wa kata ya Masama Kusini na kata ya Romu wameiomba serikali ya kata kutatua changamoto za maji ya umwahiliaji iliyodumu kwa muda mrefu.

Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro

Wananchi wa Kata za Romu na Masama Kusini wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro wameeleza kuondokana na adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji ya umwagiliaji iliyosababishwa na ubaguzi katika ugawaji wa maji kwenye mifereji ya umwagiliaji katika maeneo yao.

Wananchi hao wamesema changamoto hiyo imetokana na baadhi ya viongozi wanaosimamia ugawaji wa maji kuwapa kipaumbele watu wenye uwezo wa kifedha, huku wakiwanyima au kuwapa maji kwa muda mfupi wananchi wasiokuwa na uwezo na kwamba baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakipeleka maji kwenye mashamba yao kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyopangwa.

Kutokana na hali hiyo, Siku ya leo Februari 05,2026 wananchi wameiomba serikali ya kata kuingilia kati na kutatua changamoto hiyo, ikiwemo kuwachukulia hatua viongozi wa mifereji na ugawaji wa maji ambao wamekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 19, wakidai kuwa uwepo wao umechangia kuendelea kwa changamoto hiyo.

Sauti za Wananchi wa kata ya Romu na Kata ya Masama Kusini wakitoa kero zao mbele ya Madiwani wa kata zote mbili.
Pichani ni wananchi wa kata ya Masama Kusini na Kata ya Romu wakiwa na madiwani wao wakiwasilisha changamoto za upatikanaji wa maji ya umwagiliaji. (Picha na Henry Keto)

Kwa upande wao, Madiwani wa Kata za Romu na Masama Kusini wamesikiliza na kupokea kero hizo, huku wakiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Aidha diwani wa kata ya Masama Kusini Cedric Benjamin Pangani, amewataka wananchi wote waliokosa maji ya umwagiliaji kufika katika ofisi za kata haraka iwezekanavyo, ili kubaini chanzo cha tatizo na kuwachukulia hatua wale wote wanaozuia upatikanaji wa maji kwa wananchi wengine.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Masama Kusini Mhe. Cedric Benjamini Pangani akizungumza baada ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kata ya Masama Kusini na kata ya Romu.

Naye Diwani wa kata ya Romu Salim Mfoy, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara moja pale ambapo sheria na taratibu za ugawaji wa maji zinapovunjwa, ili hatua stahiki zichukuliwe na haki itendeke kwa wananchi wote

Sauti ya Diwani wa Kata ya Romu Mhe. Salim Mfoy akizungumza baada ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kata ya Masama Kusini na kata ya Romu.