Boma Hai FM

Diwani Trael, Machame Kaskazini waadhimisha miaka 49 ya CCM

5 February 2026, 1:21 pm

Pichani ni Diwani wa kata ya Machame Kaskazini ambae pia ni Makamu mwenyekiti wa halmshauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya (wa tano kushoto) mganga mfawidhi kituo cha afya Kisiki (aliyevaa koti jeupe)wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) kata ya Machame Kaskazini(picha na Bahati Chume)

Katika kuadhimisha miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wananchi,wanachama pamoja na Diwani wa Kata ya Machame Kaskazini wameadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti pamoja na kutembelea wagonjwa kituo cha afya Kisiki.

Na Bahati Chume

Hai -Kilimanjaro

Wananchi wa Kata ya Machame Kaskazini  wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro wameungana kusherehekea maadhimisho ya miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kufanya zoezi la upandaji miti na kutembelea wagonjwa katika Kituo cha Afya Kisiki.

Zoezi  hilo la upandaji miti pamoja na kutembelea wagonjwa limeongozwa na Diwani wa Kata hiyo ambae pia ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Trael Mboya februari 2,2026 kwa kushirikiana na wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza miti hiyo  ili malengo ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu ya jamii yafanikishwe.

Pichani ni diwani kata ya Machame Kaskazini ambae pia ni makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya akipanda mti katika kituo cha afya Kisiki(picha na Bahati Chume)

 Hata hivyo diwani  Trael Mboya ameipongeza serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo, ikiwemo Kituo cha Afya Kisiki, na kuahidi kufanyia kazi ombi la ujenzi wa uzio ili kuhakikisha usalama wa mali na watumishi waliopo katika kituo na kwamba matumaini yake ni kuona kituo hicho kinaendelea kupanuka ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wengi.

Sauti ya Diwani kata ya Machame Kaskazini ambae pia ni makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM kata hiyo Amini Mushi amewahimiza  wananchi kutunza miti iliyopandwa na kwamba kupanda miti pekee hakutoshi, bali usimamizi makini wa kila mmoja unahitajika ili kutimiza lengo.

Nae mganga mfawidhi  wa Kituo cha Afya Kisiki Saruni Kaleya, ameishukuru serikali kwa hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya, ikiwemo kuongezwa kwa watumishi na kuwepo utaratibu wa Bima kwa wananchi, ili kuhakikisha  kila mmoja  anapata huduma kwa urahisi.

Pichani ni diwani kata ya Machame Kaskazini ambae pia ni makamu mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya(katikati) picha na Bahati Chume