Boma Hai FM
Boma Hai FM
4 February 2026, 2:14 pm

Wananchi wilaya ya Hai wamehimizwa kushirikiana na Mahakama kwa kufuata sheria na taratibu, jambo litakalosaidia kuhakikisha haki, usawa, amani na maendeleo ya jamii,Maadhimisho ya wiki ya sheria yameangazia umuhimu wa mahakama kama muhimili huru wa dola unaotoa haki kwa usawa, kuleta utulivu na kusaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao.
Na Anasta Urio
Hai-Kilimanjaro
Wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wameaswa kutoa ushirikiano kwa Mahakama kwa kufuata sheria na taratibu, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja pamoja na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko Februari 2, 2026 katika ukumbi wa mahakama ya Mwanzo Bomang’ombe, wakati akitoa risala yake kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria.
Katika hotuba yake, Bomboko ameipongeza mahakama ya wilaya ya Hai kwa utendaji kazi wenye ufanisi, haki na usawa, na kuwataka waendelee na juhudi hizo, akisisitiza kuwa mahakama ni muhimili muhimu wa dola, na bila mahakama hakutakuwepo na usawa katika jamii.
Kwa upande wake Hakimu mfawidhi mahakama ya wilaya ya Hai Julieth Mawole, ameeleza kuwa mahakama inaendelea kuchukuwa hatua mbalimbali za kuboresha utoaji haki kwa kupunguza mlolongo wa kesi ,kuimarisha maadili ya utumishi nakutoa elimu ya kisheria kwa wananchi ili kuwasaidia kutambua haki na wajibu wao.
Aidha, mwanasheria wa Kujitegemea Engelbert Boniphace, amesema mahakama ni muhimili unaojitegemea, hivyo haitakiwi kuingiliwa na mihimili mingine, ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Boniphace ameongeza kuwa mahakama ina mchango mkubwa katika kuleta amani na utulivu kwenye jamii, kupitia utatuzi wa migogoro mbalimbali ya madai na jinai kwa haki na kwa wakati.