Boma Hai FM
Boma Hai FM
19 January 2026, 1:25 pm

Baada ya wananchi wa kijiji cha Nronga kupitia changamoto ya muda mrefu ya ubovu wa miundombinu ya barabara kwa sasa hawana changamoto tena baada ya barabara ya Kalali – Nronga kujengwa kwa kiwango cha zege na kuzinduliwa rasmi na Diwani wa Kata ya Machame Magharibi Martin Munisi.
Na Elizabeth Mafie na Henry Keto
Hai-Kilimanjaro
Wananchi wa Kijiji cha Nronga, Kata ya Machame Magharibi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wameondokana na adha ya muda mrefu ya miundombinu mibovu mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kalali – Nronga iliyokuwa kero kwa miaka mingi, hususan wakati wa mvua, hali iliyokuwa ikiwalazimu kutembea umbali mrefu kufuata barabara mbadala.

Wananchi wameeleza furaha yao wakisema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri na usafirishaji, kuokoa muda, kupunguza gharama za maisha pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo na kuwafikia kwa urahisi huduma muhimu.
Akizungumza mara baada ya kuzindua rasmi barabara hiyo, Diwani wa Kata ya Machame Magharibi, Mh Martin Munisi, amesema awali barabara hiyo ilikuwa korofi kiasi cha kusababisha ajali na hata kupoteza maisha, huku wananchi wakilazimika kuzunguka umbali mrefu ili kufika mjini kutokana na ubovu wake.
Munisi ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo, huku akiomba kukamilishwa kwa Mita 200 zilizosalia ili barabara hiyo itumike kikamilifu kwa mwaka mzima, jambo litakalowezesha wananchi wa Machame Magharibi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi na usalama zaidi.


Akizungumza kwa niaba ya meneja wa TARURA wilaya ya Hai Mhandisi Christopher Deogratius amesema ujenzi wa barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 6 katika maeneo ya milimani ya Kalali Nronga, pamoja na uwekaji wa mitaro na tabaka la zege katika mita 400, huku zilizotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 448, fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Hai.