Boma Hai FM

Dc Bomboko ahimiza utatuzi wa kero za wananchi kwa vitendo

17 January 2026, 8:11 am

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko (katikati)akiwa katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Snow View(picha na Riziki Lesuya)

Malalamiko ya wananchi wilaya ya Hai yanaendelea kupungua, hali inayotajwa kuchangiwa na juhudi za uongozi wa wilaya hiyo kusikiliza na kutatua kero moja kwa moja kwa wananchi.

Na Oliva Joel

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Hassan Omary Bomboko, amesema kuwa utatuzi wa kero za wananchi kwa kuzisikiliza na kuzifanyia kazi moja kwa moja katika kata zote za wilaya hiyo, umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la malalamiko linalojitokeza mara kwa mara katika jamii.

Bomboko ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Snow View vilivyopo Kata ya Bomang’ombe, mkutano uliowakutanisha zaidi ya wananchi mia moja pamoja na wakuu wa vitengo, wataalamu na watumishi wa kada mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko.

Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku, zikiwemo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama, miundombinu ya barabara, huduma ya umeme pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Sauti za wananchi waliotoa kero zao katika mkutano wa hadhara.

Baada ya kusikiliza kero hizo, Mkuu wa Wilaya ya Hai amewataka watumishi wote wa umma wilayani humo kuongeza uwajibikaji kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao, badala ya kusubiri malalamiko yaandikwe, ili changamoto zinazojitokeza zipatiwe ufumbuzi wa haraka na wa vitendo.

Pichani ni mwanachi wa wilaya ya Hai akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya snow view (picha na Riziki Lesuya)

Sambamba na hilo Bomboko amesisitiza suala la nidhamu kazini kwa watumishi wa Halmashauri akiwataka kufika kazini kwa wakati, kutekeleza majukumu yao ipasavyo, na kuondoka mara baada ya kumaliza kazi, huku akibainisha kuwa uzembe kazini hautavumiliwa.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko.

Mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa Wilaya ya Hai wa kusogeza huduma karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao moja kwa moja, na kuhakikisha kero zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa lengo la kuboresha ustawi wa jamii.

Pichani ni mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya snow view(picha na Riziki Lesuya)