Boma Hai FM
Boma Hai FM
1 December 2025, 1:26 pm

Jamii yaaswa kuachana na mitazamo hasi dhidi ya watoto wenye mahitaji maalumu.
Na Elizabeth Mafie Hai -Kilimanjaro
Jamii imetakiwa kuondoa mitazamo hasi ya kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu, kwani watoto hao wana uwezo wa kujitegemea na kusimama wenyewe iwapo watapata elimu na usimamizi unaostahili.

Wito huo umetolewa na afisa elimu maalum walaya ya Hai Hidaya Kilima, katika hafla ya wahitimu wa ujuzi mbalimbali iliyofanyika katika Kituo cha Gabriella Children Rehabilitation Centre (GCRC) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro amesema kuwa, watoto wenye mahitaji maalumu wana uwezo mkubwa wa kufika mbali endapo wataungwa mkono ipasavyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Brenda Shuma, amesema licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kuwahudumia watoto na vijana hao, bado kuna uhitaji wa misaada mbalimbali ikiwemo usafiri, vifaa tiba, vifaa vya kujifunzia na rasilimali nyingine muhimu.
Kwa upande wa wazazi Tegemea Mfanga ametoa wito kwa wazazi wenzake kuwa mabalozi wazuri wa kutetea haki za watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwatoa na kuwapeleka kupata elimu badala ya kuwaficha nyumbani.
Mmoja wa vijana waliohitimu mafunzo katika kituo hicho ameahidi kutumia ujuzi aliojifunza kujitegemea, kusaidia familia yake na kuendelea kufuatilia ndoto zake, huku akilishukuru kituo kwa malezi na mafunzo wanayopata.
Kituo cha Gabriella kinaendelea kuwawezesha watoto na vijana wenye ulemavu kupata ujuzi na stadi mbalimbali ili wawe huru na wanaokubalika katika jamii.

Pichani ni afisa elimu maalumu wilaya ya Hai Hidaya Kilima akimkabidhi cheti mwanafunzi aliyehitimu(picha na Elizabeth Mafie)