Boma Hai FM
Boma Hai FM
30 November 2025, 12:11 pm

Wananchi wa Kijiji cha Rundugai wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wamefurahia na kuishukuru Serikali baada ya kupokea shilingi milioni 85 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madrasa na kituo kidogo cha polisi, miradi inayotarajiwa kuboresha elimu na usalama katika eneo hilo.
Na Bahati Chume Hai-Kilimanjaro
Wananchi wa Kijiji cha Rundugai wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wameishukuru Serikali kwa kuwaletea miradi miwili ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 85.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vyumba viwili vya madrasa kwa ajili ya shule maalumu ya watoto wenye ulemavu (sh milioni 65.3) pamoja na shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha polisi.
Shukrani hizo zimetolewa Novemba 28, 2025 wakati wa mkutano maalumu wa kijiji ulioitishwa kujadili utekelezaji wa miradi hiyo na namna wananchi watakavyoshiriki nguvu kazi ili ikamilike kwa wakati.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, wananchi wamesema miradi hiyo inaonesha wazi jinsi Serikali inavyowajali.
Kwa upande wake Kimangalu Mdee amesema ujenzi wa kituo cha polisi ni muhimu kutokana na changamoto za kiusalama katika ukanda huo, ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji , Amesema wananchi wako tayari kutoa ushirikiano, ikiwemo kukusanya mawe na kuchimba msingi ili mradi uanze mara moja.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Beda Msofe amesema miradi yote miwili imepokelewa rasmi na kazi za awali ikiwa ni uchimbaji wa msingi na uandaaji wa vifaa zitaanza mara moja kuanzia Novemba 29, 2025.
Afisa Tarafa wa Masama Nsajigwa Ndagile, amewataka viongozi wa kijiji kusimamia miradi hiyo kwa karibu ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma ,Ameongeza kuwa ulinzi na amani ni jambo la msingi, akiwahimiza vijana kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa eneo hilo.