Boma Hai FM
Boma Hai FM
28 November 2025, 5:15 pm

Siku ya Lishe Kitaifa huadhimishwa kila mwaka nchini Tanzania ili kukumbusha dhana ya haki ya kupata chakula bora, kupambana na udumavu, na kuhimiza uwekezaji katika afya dhamira inayokwenda sambamba na mpango wa taifa wa kuboresha lishe ulioanzishwa miaka kadhaa iliyopita.
Na James Gasindi Hai -Kilimanjaro
Maadhimisho ya Siku ya Lishe kitaifa yamefanyika Kiwilaya leo katika Kituo cha Afya Masama kilichopo Kata ya Romu wilayani Hai, yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kama msingi wa afya na maendeleo ya kiuchumi.
Siku ya Lishe Kitaifa huadhimishwa kila mwaka nchini Tanzania ili kukumbusha dhana ya haki ya kupata chakula bora, kupambana na udumavu, na kuhimiza uwekezaji katika afya dhamira inayokwenda sambamba na mpango wa taifa wa kuboresha lishe ulioanzishwa miaka kadhaa iliyopita.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesema taifa linategemea wananchi kama nguvu kazi lakini mchango huo hauwezi kutimia bila afya bora. Amesema afya njema huanzia kwenye uchaguzi sahihi wa chakula na namna jamii inavyojenga utamaduni wa ulaji unaozingatia virutubisho muhimu. Ameeleza kuwa suala la lishe limekuwa ajenda ya muda mrefu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu akiwa Makamu wa Rais na hadi sasa akiwa madarakani ameendelea kulipa kipaumbele ili kupunguza changamoto za kiafya katika jamii.
Bomboko amesema katika kipindi cha miaka mitano, serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 11 katika sekta ya afya wilayani Hai, uwekezaji unaoonekana katika ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na ufikishaji wa huduma kwa wananchi. Amesema jamii inapaswa kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kuanzia majumbani hadi mashuleni na wazazi kufuatilia chakula kinachotolewa shuleni ili kujiridhisha kuwa kina ubora unaohitajika.
Amesema maeneo mengi ya wilaya hiyo yana uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa mazao na matunda mbalimbali hivyo wananchi hawana sababu ya kukosa lishe bora nakuonya kuwa ulaji usiozingatia virutubisho unaweza kusababisha magonjwa sugu yanayoweza kuathiri vizazi vinavyofuata na kuongeza gharama kubwa za matibabu. Katika tathmini ya wilaya, ameweka wazi kuwa bado kuna asilimia 32 ya watoto wenye udumavu jambo linaloonyesha uwepo wa pengo la uelewa na uhitaji wa kampeni endelevu za lishe.

Afisa Lishe wa Wilaya ya Hai Silvania Kulaya amesema wanaume wanapaswa kushiriki kikamilifu katika shughuli za lishe kwa kuwa wao ndio waamuzi wakuu katika matumizi ya rasilimali za familia. Amesema halmashauri imeendelea kuanzisha programu za lishe, kutoa elimu katika vituo vya afya, mashuleni na kwenye makundi ya kijamii ili kupunguza changamoto za utapiamlo kwa watoto na wanawake.
Baadhi ya wananchi akiwemo Juleth Swai, Mc Shuma na Zaina Mushi wamesema elimu waliyopata imewasaidia kubaini makosa waliyokuwa wakiyafanya katika mfumo wao wa ulaji. Wamesema mara nyingi wamekuwa wakila kwa mazoea bila kuzingatia virutubisho vinavyohitajika na sasa wameamua kubadilika na kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu lishe bora.
Maadhimisho ya mwaka huu yameendelea kuikumbusha jamii kuwa lishe sio suala la anasa bali ni nyenzo ya msingi ya kujenga taifa lenye afya, nguvu kazi imara na uchumi endelevu yakiwa na kauli mbiu inayosema afya ni mtaji wako zingatia unachokula.