Boma Hai FM

Saashisha akutana na waendesha pikipiki na bajaji Hai

26 November 2025, 9:12 am

Pichani ni Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe(kulia)na kiongozi wa madereva bajaji wilaya ya Hai Baraka Ngoti(picha na Praygod Munisi)

Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amekutana na madereva pikipiki na bajaji wa wilaya ya Hai kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili.

Na Elizabeth Mafie

Maofisa wasafirishaji wa pikipiki na bajaji katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro waomba kujumuishwa katika mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ili nao wawe miongoni mwa wanufaika wa fedha za Serikali zinazolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Pichani ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe akizungumza na madereva pikipiki na bajaji wilaya ya Hai katika ukumbi wa polisi Hai(picha na Praygod Munisi)

Ombi  hilo limetolewa   katika kikao cha kujadili na kutatua changamoto zao kilichofanyika katika ukumbi wa Polisi wilayani Hai,  Novemba 24,2025 wakikutana na Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

Vijana hao wanaeleza kuwa licha ya kuwepo kwa mikopo ya Halmashauri, bado kundi lao halijaonekana kunufaika, hivyo wanaomba kuangaliwa kama sehemu ya makundi yanayostahili kupata mikopo hiyo.

Sauti ya Kiongozi wa madereva pikipiki wilaya ya Hai Ombeni Lema.

Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe amefafanua kuwa sheria inaelekeza asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kugawanywa kwa makundi maalum: asilimia 4 kwa vijana, asilimia 4 kwa kina mama, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe

Saashisha amesisitiza kuwa lengo la mikopo hiyo  ni kuongeza uwezo wa wananchi kujikwamua kiuchumi, na kwamba upo umuhimu  wa vijana wa sekta ya usafirishaji kupata nafasi ya kukopeshwa ili kuimarisha shughuli zao.

Pichani ni madereva bajaji na pikipiki wa wilaya ya Hai wakiwa katika kikao na mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe(hayupo pichani) picha na Praygod Munisi