Boma Hai FM
Boma Hai FM
23 November 2025, 9:32 am

Pichani ni Mwenyekiti wa Hai Teachers Saccos Baraka Owenya katika mkutano mkuu wa mwaka 2025 uliofanyika katika viwanja vya Saccos hiyo vilivyopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro( picha na Elizabeth Mafie)
Hai Teachers Saccos yafanya mkutano mkuu wa mwaka 2025 ,yaweka maazimio mezani wakubaliana kupandisha Hisa.
Na Elizabeth Mafie
Chama cha akiba na mikopo Hai Teachers SACCOS kimefanya mkutano mkuu wa ishirini na tano Novemba 22, 2025 katika viwanja vya SACCOS hiyo vilivyopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Bi. Hellen Mwambeta ndiye mgeni rasmi na ametoa pongezi kwa uongozi wa SACCOS hiyo kwa kazi kuu ya kuwawezesha watumishi na kuimarisha ustawi wao kiuchumi.
Wanachama wawakilishi walioshiriki mkutano huo wamepitisha maazimio mbalimbali kwa mwaka 2026, yakiwemo kupandisha kiwango cha hisa kutoka 50 hadi 100 kwa mwanachama, pamoja na kuwepo kwa tuzo maalum kwa wawekezaji bora katika maeneo ya Akiba, Amana na Hisa.

Mwenyekiti wa Hai Teachers SACCOS, Baraka Owenya, amewasilisha malengo ya taasisi hiyo kwa sasa na kwa miaka ijayo, likiwemo lengo la kuongeza idadi ya wanachama kutoka 1,835 hadi kufikia 2,000 ifikapo Desemba 2026. Uongozi pia umeweka mkakati wa kuboresha sera mbalimbali pamoja na mpango wa kupunguza kiwango cha riba ya mikopo kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 ifikapo mwaka 2028.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Hai Teachers SACCOS, Beatrice Msuya, amewasilisha makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2026, ambayo yamejadiliwa na kisha kupitishwa kama mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa mwaka ujao.

Hai Teachers SACCOS ilianzishwa mwaka 1993 ikiwa na wanachama 20 pekee na mtaji wa shilingi 100,000. Hadi kufikia sasa taasisi hiyo inahudumia wanachama 1,825 na ina mtaji unaozidi shilingi bilioni 2, ikionesha maendeleo makubwa ya kihistoria tangu kuanzishwa kwake.
