Boma Hai FM
Boma Hai FM
28 September 2025, 9:01 am

Katika kutekeleza msingi wa tano wa vyama vya ushirika wa Elimu ,mafunzo na taarifa Hai Teacher’s Saccos wafanya mkutano na kukusanya dondoo zitakazotumika katika mkutano mkuu wa mwaka 2025.
Na Elizabeth Noel Hai -Kilimanjaro
Chama cha Akiba na Mikopo cha Hai Teacher’s Saccos kimefanya mkutano wa wanachama kwa lengo la kukusanya dondoo zitakazojadiliwa katika mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2025.

Mkutano huo umefanyika Septemba 27, 2025 katika ofisi za Saccos hiyo zilizopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na mamia ya wanachama.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mwenyekiti wa Hai Teacher’s Saccos Baraka Owenya, amesema mkutano huo ni utekelezaji wa msingi wa tano wa vyama vya ushirika wa elimu,mafunzo na taarifa na kwamba ulikuwa ni fursa ya wanachama kutoa maoni na mapendekezo kwa lengo la kufanya maboresho na kuandaa mpango wa muda mrefu wa kukuza chama.
“Wanachama wamepata nafasi ya kufahamu mambo yanayoendelea katika chama chao pamoja na mafanikio yaliyopatikana,” Amesema Owenya.
Naye Meneja wa Saccos hiyo, Beatrice Msuya, amefafanua kuwa chama hicho kilianzishwa mwaka 1993 kikiwa na wanachama waanzilishi 40 pekee na mtaji wa shilingi 100,000, na kwamba Hadi sasa, Saccos hiyo imekua na kufikia zaidi ya wanachama elfu moja na mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Beatrice ameongeza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana kupitia ongezeko la wanachama na mtaji, huku akisisitiza kuwa mkakati wa sasa ni kuendelea kukuza mtaji huo sambamba na kuboresha huduma kwa wanachama.

“Tunawaalika watumishi wa serikali ambao bado hawajajiunga na Hai Teacher’s Saccos kufanya hivyo mara moja, kwani wanakosa fursa nyingi za kiuchumi,” Amesema Beatrice.
Radio Boma Hai FM pia ilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wanachama akiwemo Mwalimu Antuswa Lyakurwa na Mwalimu Anjela Julius, ambao walieleza kufurahishwa na mkutano huo na jinsi walivyonufaika kupitia huduma za Saccos hiyo.
Kwa upande wake Edwin Donath mwanachama mpya wa chama hicho, amesema kuwa kujiunga na Saccos hiyo kumemsaidia kutimiza malengo yake ya kifedha mapema kuliko alivyotarajia.