Boma Hai FM

Nanenane nguzo kwa wakulima na wafugaji

6 August 2025, 7:01 pm

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga akiwa na Mkuu wa Mkoa wa kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu pamoja na viongozi wengine katika ufunguzi wa sherehe za maonyesho ya nanenane viwanja vya temi mkoani Arusha(Picha na Henry Keto)

Maadhimisho ya 31 ya sherehe za maonyesho ya nanenane yamefunguliwa Agosti 5,2025 kwenye viwanja vya temi njiro mkoani Arusha na mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu

Na Salma Rahim-Arusha

Wakulima na wafugaji kanda ya kaskazini kwenye mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro wameaswa kutumia Kilimo cha kisasa chenye tija kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na Kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazo na Mifugo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga ambaye ndiye Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa sherehe ya 31 ya nanenane kanda ya kaskazini akiambatana na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, ufunguzi huo imefanyika August 5,2025 kwenye viwanja vya temi mkoani Arusha yenye Kauli mbiu isemayo “Kwa maendeleo bora ya Kilimo, ufugaji na uvuvi, Chagua viongozi bora 2025”

Katika hotuba yake ya kufungua maadhimisho ya nane nane, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga asisitiza umuhimu wa wakulima na wafugaji kutumia mbegu bora ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na mifugo, Ameeleza kuwa matumizi ya mbegu bora ni msingi wa kilimo chenye tija na chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Queen Sendiga akizungumza wakati wa ufunguzi wa nanenane Arusha

Pia, amehimiza wananchi kuonyesha utayari wa kupokea mabadiliko yanayoletwa na wataalamu wa kilimo na mifugo akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufikiwa bila kukubali maarifa mapya kutoka kwa wataalamu waliobobea, na akiwasihi wataalam hao kuhakikisha elimu wanayoitoa inawafikia wananchi wa ngazi zote ili kuleta kilimo na ufugaji wenye tija kwa maendeleo.

Vile vile,mkuu wa Mkoa Manyara amepongeza mchango mkubwa wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo, ambapo amebainisha kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 139 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya umwagiliaji katika mikoa mitatu ya kaskazini kwani hatua hii ni muhimu sana kwa kuzingatia kuwa kilimo ndicho kiini cha maisha ya wengi nchini, hasa wakulima wengi waliopo vijijini.

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi wengine wakitembelea mambanda na vitalu vya kilimo kwenye ufunguzi wa maonyesho ya nanenane Arusha (Picha na Henry Keto)

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe Nurdini Babu katika maonesho hayo ya kufungua sherehe za nane nane , amewaasa wananchi kuhakikisha kuwa wanachagua viongozi waadilifu na wenye sifa zinazostahili ili kuimarisha utawala bora na maendeleo endelevu katika jamii, Mhe. Babu pia alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha usalama na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Vilevile Mhe Nurdin Babu amesema kuwa mkoa wa Kilimanjaro uko katika hali ya amani na usalama wa kuridhisha ambapo alisisitiza kuwa usalama huu unachangia maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mkoa huo aidha, Babu alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha mazingira ya amani yanadumu, ili kila mtu aweze kufanikisha shughuli zake bila wasiwasi wowote. Hali hii ya usalama inajenga imani kwa wawekezaji na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu akizungumza wakati wa ufunguzi wa nanenane Arusha

Aidha, Afisa kilimo wilaya ya Hai Saudi Ngura ameeleza umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa katika kilimo cha mboga mboga, kama umwagiliaji wa matone unaosaidia kuokoa maji na kuongeza tija mashambani na pia matumizi ya mbolea ya kisasa inavyosaidia katika kuongeza rutuba ya udongo, nakutoa wito Kwa wakulima kutembelea mabanda ya maonesho ili kujifunza teknolojia mpya na mbinu bora za kilimo kutoka kwa wataalam ili kuongeza uzalishaji.

Sauti ya Afisa Kilimo wilaya ya Hai Saudi Ngura akizungumza kuhusu teknolojia wanayotumia kwenye kilimo cha mbogamboga kwenye maonyesho ya nanenane Arusha

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu akipewa maelezo kuhusu bidhaa ndani ya banda la wilaya ya Hai,(Picha na Henry Keto)

Sikukuu ya maonyesho ya wakulima na wafugaji (nanenane) kwa kanda ya kaskazini yanaendelea kwa kipindi cha siku nne mpaka tarehe 8 ambapo ndio kilele cha maadhimisho hayo ambapo Wananchi kutoka maeneo mbalimbali wanaalikwa kushiriki na kujionea pamoja na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu Kilimo na ufugaji pamoja na maonyesho ya bidhaa mbalimbali kwenye mabanda yaliyopo ndani ya uwanja wa temi mkoani Arusha.