Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 July 2025, 9:34 am

Chama cha akiba na mikopo Hai Rural Teachers Saccos (HRT) kimefanya Bonanza la aina yake katika viwanja vya Taasisi ya Charllote katika kuelekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.
Na Elizabeth Noel Siha-Kilimanjaro
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Akiba na Mikopo Hai Rural Teachers Saccos chama hicho kimeandaa bonanza kubwa la michezo lililofanyika Julai 19, 2025 katika viwanja vya Taasisi ya Charlotte wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Bonanza hilo limewakutanisha wanachama kutoka wilaya za Hai na Siha, ambapo walishiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa mikono, na mpira wa pete.
Katika matokeo ya michezo hiyo, timu ya mpira wa miguu kutoka Siha iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu ya Hai. Hata hivyo, kwenye mpira wa mikono, timu ya Hai walirejesha heshima kwa ushindi wa pointi 2-1, huku wakitawala kabisa mchezo wa mpira wa pete kwa kuwachapa Siha kwa mabao 21-0.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo Mwenyekiti wa HRT SACCOS, Mwalimu Alex Warioba amesema kuwa bonanza hilo ni sehemu ya shughuli za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya chama hicho, yaliyopangwa kufanyika rasmi Julai 26, 2025 katika viwanja vya Chuo cha Ufundi KKKT wilayani Hai.

“Tuko kwenye uzinduzi wa bonanza kuelekea maadhimisho ya miaka 25 ya HRT SACCOS tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000. Leo tuna bonanza la michezo, lakini pia Jumanne ya tarehe 22 Julai tutakwenda shule ya Ngaremji kutoa madawati kama sehemu ya kurudisha kwa jamii hili ni mojawapo ya malengo ya vyama vya ushirika, kama inavyoelezwa kwenye kanuni ya saba ya ushirika faida irudi kwa jamii,” amesema Mwalimu Warioba.
Naye Meneja wa HRT SACCOS, Bi. Upendo Lyatuu ameeleza kuwa bonanza hilo limeandaliwa kwa lengo la kudumisha mshikamano baina ya wanachama wa wilaya zote mbili akikumbusha kuwa mwaka 2007 ambapo wanachama wa Siha walitaka kuanzisha Saccos yao baada ya kutenganishwa kiutawala na wilaya ya Hai, lakini HRT SACCOS iliweza kuwahamasisha kubaki pamoja na kuendeleza umoja wao.

“Leo tumeonesha mshikamano wetu kupitia michezo hili ni jambo muhimu na tunakusudia kufanya mabonanza haya kuwa ya kila mwaka, ili kuwahamasisha wengine kujiunga na HRT SACCOS,” amesema Bi. Lyatuu.
Baadhi ya wanachama walioshiriki, akiwemo Abdulbast Hamis na Mwalimu Marium Hery wakaeleza furaha yao kushiriki bonanza hilo, huku wakielezea namna chama hicho kilivyowanufaisha kiuchumi na kuwasaidia katika maendeleo ya maisha yao.
Mwalimu Marium Hery akaenda mbali zaidi na kusema kwamba kwa zamani ilikuwa si rahisi kwa mwalimu kumiliki vyombo vya usafiri pamoja na nyumba za kisasa lakini kwa sasa kupitia HRT SACCOS wanamiliki mali hizo.
Hadi sasa HRT SACCOS imeendelea kufanya vizuri tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ikiwa na wanachama waanzilishi 67 pekee,na sasa ikijivunia kuwa na wanachama zaidi ya 2,000 ishara tosha ya imani ya wanachama na uongozi madhubuti wa chama hicho kwa miaka 25.