Boma Hai FM
Boma Hai FM
18 July 2025, 9:09 am

“Mtoto huyo alikuwa akiishi na bibi yake na kusoma darasa la kwanza mara nyingi akirudi nyumbani anakuwa peke yake kwa kuwa bibi yake anakuwa katika shughuli za kujitafutia riziki hivyo mshitakiwa kwa kuwa walikuwa majirani, alitumia nafasi hiyo kutenda unyama huo,” amesema Chishimba.
Na Elizabeth Noel Siha- Kilimanjaro
Mkazi wa Kijiji cha Wandri wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Agust Shoo maarufu kama Baba Steven (59) amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa mawili ya kubaka na kulawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 6.
Hukumu hiyo imetolewa Julai 15, 2025 na Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Siha, Jasmine Abduli, kesi hiyo, namba 20095/2023, imesikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi watano wakiwemo muhanga mwenyewe, daktari, na mama mzazi wa mtoto.
Katika kosa la kwanza la ubakaji, mshitakiwa alipatikana na hatia kwa mujibu wa Kifungu cha 130(1)(2)(e) na Kifungu cha 131(1) cha Sheria ya makosa ya Jinai, Sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, ambapo amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Kwa kosa la pili la kulawiti, mshitakiwa amepatikana na hatia kwa mujibu wa Kifungu cha 154(1)(a) cha Sheria ya makosa ya jinai, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022, ambapo adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, David Chishimba, ameeleza mahakama kuwa tukio hilo lilitokea kwa nyakati tofauti mnamo Oktoba 8, 2019 katika kijiji hicho, ambapo mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa kumbaka na kumlawiti mtoto huyo huku akitambua wazi kuwa ni kosa.
Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitumia nafasi ya ukaribu wao kama majirani kufanya ukatili huo kwa kumrubuni mtoto huyo kwa zawadi, akitumia mwanya wa bibi wa mtoto kuwa hayupo nyumbani wakati mtoto anarudi kutoka shule.
“Mtoto huyo alikuwa akiishi na bibi yake na kusoma darasa la kwanza mara nyingi akirudi nyumbani anakuwa peke yake kwa kuwa bibi yake anakuwa katika shughuli za kujitafutia riziki hivyo mshitakiwa kwa kuwa walikuwa majirani, alitumia nafasi hiyo kutenda unyama huo,” amesema Chishimba.
Tukio hilo liligundulika baada ya mtoto huyo kufika shuleni akiwa katika hali isiyo ya kawaida, ambapo haja kubwa ilimvuja bila kujitambua, na kusababisha wenzake kumcheka ndipo mwalimu wake alimtambua na kumhoji, na mtoto huyo kueleza yaliyomsibu pamoja na mtoto huyo kumtaja mshitakiwa.
Baada ya kusikiliza ushahidi pande zote mahakama iliridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa haukuwa na shaka na hivyo kumhukumu mshitakiwa kutumikia kifungo cha maisha jela .