Boma Hai FM
Boma Hai FM
10 June 2025, 9:08 pm

Ufunguzi wa mafunzo ya Jeshi la akiba katika kijiji cha Kware kata ya Masama Kusini wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro
Na James Gasindi. Hai-Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Haasan Bomboko, amewataka vijana waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa mfano wa uzalendo, uaminifu, na nidhamu ndani ya jamii wanazotoka, huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua ya awali ya kuandaliwa kwa ajili ya kulitumikia taifa.
Akizungumza katika kijiji cha Kware leo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa vijana, DC Bomboko alisema kuwa nafasi hiyo si ya kawaida, bali ni mwito wa kuitumikia nchi kwa uadilifu na moyo wa kujitoa, pia amewaasa kuwa askari wa Jeshi la Akiba anatakiwa awe mtu anayeaminika na kukubalika na jamii, na kamwe hawezi kupata heshima hiyo bila kuwa muadilifu.

Katika maelezo yake, Bomboko aliweka wazi kuwa sifa ya kwanza kwa mwanajeshi ni nidhamu, na kwamba mtu asiye na nidhamu hawezi kuwa askari. Alionya dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu au kuwalinda wahalifu, akisema hilo linakiuka misingi ya maadili ya kijeshi, aidha aliwataka vijana hao kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
DC Bomboko aliwataka vijana kutumia kipindi chote cha mafunzo kujijenga kiakili na kiroho ili kuwa raia bora, akisisitiza kuwa maarifa yatakayopatikana yasitumike vibaya, bali yatumike kwa faida ya jamii.