Boma Hai FM

Saashisha azindua zahanati ya milioni 121

5 June 2025, 9:36 pm

Pichani ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Elinikyo Mafuwe akipokelewa na wananchi wa kata ya Bondeni wakati alipofika kwa ajili ya kuzindua zahanati kijiji cha Lerai.(picha na Elizabeth Mafie)

Wananchi wa kata ya Bondeni kijiji cha Lerai waipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

Na Elizabeth Mafie. Hai-Kilimanjaro

Wananchi wa Kijiji cha Lerai kata ya Bondeni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro,wameondokana na kadhia ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya baada ya kukamilika kwa zahanati kijijini hapo.

Akizindua Zahanati hiyo iliyo gharimu kiasi cha shilingi Milioni 121 Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amesema kuwa kukamilika kwa Zahanati hiyo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kutawasaidia kuepuka kutembea umbali mrefu badala yake kutumia muda mfupi na kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Pichani ni Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe (aliyevaa shati la drafti)akizindua zahanati ya Lerai(picha na Elizabeth Mafie)

Mbali na kuzindua zahanati hiyo Mbunge Saashisha  ametumia nafasi hiyo kudhibitisha kwa wananchi kuwa changamoto wanazo mtuma anazisemea bungeni ili kupata majibu kwa kuwasikilizishia wananchi alivyo uliza swali bungeni Juni 5,2025 kuhusu upatikanaji wa kituo cha afya ndani ya kata hiyo ya Bondeni.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

Kwa Upande wake diwani wa kata ya Bondeni Vincent Mamasitta ameshukuru kukamilika kwa ujenzi huo huku akimuomba Mbunge huyo kuwezesha upatikanaji wa Kituo Cha Afya kama walivyo msikia Bungeni kwani Kata hiyo imekidhi vigezo vyote vya kuwa na Kituo Cha Afya kama inavyohitajika.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo ya Lerai mganga mfawidhi wa zahanati Jeremiah Kubuguta  amesema kuwa zahanati hiyo inahudumia zaidi ya vijiji vitatu huku akiomba changamoto ya uhaba wa watumishi,kichomea taka,nyumba za watumishi na wodi ya kujifungulia kutatuliwa ili kuendelea kurahisisha utoaji wa huduma.

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji hicho akiwemo Saumu Saidi na Edward Kaaya wamemshukuru Mbunge Saashisha kwa kufanikisha ujenzi wa Zahanati hiyo baada ya kukosa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Sauti za wananchi wa kata ya Bondeni.

Uwepo wa vituo vya afya na zahanati ndani ya Jimbo la Hai kunawawezesha wananchi wenye kipato kidogo kumudu gharama,kuwezesha utoaji wa huduma za uzazi, kliniki za wajawazito, ushauri wa lishe na chanjo kwa watoto wachanga pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Pichani ni jengo la zahanati lililozinduliwa na Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe(picha na Elizabeth Mafie)