Boma Hai FM

Saashisha: Hili shamba ni letu na hilo halina mjadala

2 June 2025, 9:16 pm

Pichani ni Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Elinikyo Mafuwe (aliyevaa kofia)pamoja na mkuu wa wilaya ya Hai(katikati) na diwani wa kata ya Machame Kaskazini Judica Kwayu wakizungumza na wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kukabidhiwa shamba kutoka kwa mwekezaji Elizabeth Stegmaier (picha na Elizabeth Mafie)

Hatimaye mgogoro wa shamba uliodumu kwa miaka 26 kati ya mwekezaji   Elizabeth  Stegmaier na chama cha  msingi cha ushirika Uduru Makoa  lenye ukubwa wa hekari 358 unatarajiwa kumalizika mara baada ya hatua za kisheria kukamilika.

Na Elizabeth Mafie-Hai Kilimanjaro.

Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amewataka wananchi wa kata ya Machame Kaskazini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kuwa wavumilivu  katika kupata haki yao ya kukabidhiwa shamba la Makoa linalomilikiwa na chama cha ushirika uduru  Makoa  kutoka kwa mwekezaji  Elizabeth  Stegmaier na kwamba shamba hilo ni haki yao na mahamakama kuu imethibitisha kwamba shamba hilo ni la wananchi.

Saashisha ameyasema hayo leo Juni 2, 2025  wakati akizungumza na wananchi  waliojitokeza kwa ajili ya kukabidhiwa shamba kutoka kwa mwekezaji huyo anayedaiwa kukiuka mkataba wa shamba hilo na kulitumia kwa manufaa yake binafsi kwa miaka ishirini na sita.

Aidha Saashisha amewasihi wananchi hao kutofanya vurugu yoyote na kuwa  watulivu kwani kukosea hatua moja kutampa nafasi mwekezaji huyo kuendelea kuwasumbua hivyo ni vyema kuendelea kuheshimu muhimili wa mahakama na kwamba  jambo likiwa mahakamani zipo taratibu zakufuata.

“Cha kwanza hili ni shamba letu, ni haki yetu hilo halina mjadala lakini pia mahakama kuu imetuthibitishia kwenye hukumu yake kuwa shamba hili ni la kwetu hilo halina mjadala,lakini lenye mjadala ni hatua za makabidhiano,hatua hizi za makabidhiano tukikosea hatua moja tunampa nafasi ya yeye kuendelea kutusumbua, tunaheshimu muhimili wa mahakama,jambo likiwa mahakani kuna namna yake kuna taratibu zake,hivyo kuweni watulivu” Amesema Saashisha.

Pichani ni wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kukabidhiwa shamba hilo(picha na Elizabeth Mafie)

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesema mgogoro huo umepitia hatua tofauti tofauti lakini siku za hivi karibuni mahakama kuu imetoa maamuzi yanayoonyesha hakuna mkataba na mwekezaji huyo na kwamba shamba hilo linatakiwa kurudi katika chama cha  msingi cha Ushirika cha Uduru.

 Bomboko ameeleza kuwa tayari chama hicho cha msingi cha ushirika Uduru kimempata taarifa mwekezaji huyo ya kumtaka aondoke katika eneo hilo.

“Ndugu zangu mgogoro huu umepitia hatua tofauti tofauti lakini siku za hivi karibuni mahakama kuu imetoa maamuzi ambayo inaonyesha kabisa hakuna mkataba kwa sasa na eneo hili lirudi kwa ushirika” Amesema Bomboko.

Nao wananchi waliojitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutaka kukabidhiwa shamba hilo wakapata nafasi ya kumshukuru Mbunge wa jimbo la Hai kwa namna alivyopambana kurejesha shamba hilo kwa wananchi.

Sauti ya mwananchi wa kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini Anzamen Jeremia Mbowe.