Boma Hai FM

RC Babu akemea wanaodharau zao la kahawa

27 May 2025, 11:11 am

Pichani ni mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurduni Babu akizungumza na jukwaa la vyama vya ushirika mkoa wa Kilimanjaro(picha na Winnie Shao)

“Mazao ya kibiashara katika nchi yetu hususani zao la kahawa kwa mkoa wetu wa Kilimanjaro, tumedharau zao la kahawa, tunakata mikahawa na kujenga majumba lakini tukumbuke kwamba mikahawa hiyo ndio imewasomesha watoto wetu kufika chuo kikuu”

Na Elizabeth Mafie-Moshi Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema  zao la kahawa litabaki kuwa zao la biashara kwa mkoa wa Kilimanjaro na kwamba sio jambo jema kuondoa alama ya zao hilo kwa kuzikata na kujenga majumba.

Babu ameyasema hayo  Jumatatu Mei 26,2025  wakati akizungumza katika jukwaa la nne la wadau wa maendeleo ya ushirika mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika mjini Moshi.

“Mazao ya kibiashara katika nchi yetu hususani zao la kahawa kwa mkoa wetu wa Kilimajaro,tumedharau zao la kahawa ,tunakata mikahawa na kujenga majumba,lakini tukumbuke kwamba mikahawa hiyo ndio imewasomesha watoto wetu kufika chuo kikuu”Amesema Babu.

Sauti ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdini Babu.

Aidha Babu amesema yupo tayari kusimama pamoja na wakulima kwa kupigania haki zao ambazo zinafunjwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya Ushirika.

Mwenyekiti  wa Jukwaa la wadau wa Maendeleo ya Ushirika  mkoa wa Kilimanjaro Bosco Simba amesema uwepo wa majukwaa hayo ya Ushirika huchochea uhamasishaji na ukuaji wa ushirika katika mkoa na Nchi kwa ujumla.

Pichani ni maafisa ushirika kutoka vyama mbalimbali vya ushirika mkoani Kilimanjaro(picha na Winnie Shao)

Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro Jackline Senzighe amesema  baadhi ya wanachama wanakabiliwa na uhaba wa Maafisa Ushirika,ukosefu wa soko kuu la Kahawa na uwezo wa vyama kuhimili ushindani  ,matumizi mabaya ya  madaraka kwa uongozi na watendaji kwa kuwa na mgongano wa maslahi na kujipendelea katika utoaji wa huduma.

Bahati Yogola ni Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Kaskazini amevitaka vyama vya Ushirika  kuchangamkia fusra ya kukata bima ambayo  itawasaidia kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.

Jukwaaa hilo ni la nne kufanyika ambapo kwa mwaka huu litafanyika kwa siku mbili Mei 26 na 27,2025 ambapo washirika watajifunza mada  mbalimbali juu ya Ushirika kuelezea mafanikio na changamoto mbalimbali zilizopo  ,mikakati ya kukuza ushirika, pamoja na uchaguzi wa viongozi.