Boma Hai FM
Boma Hai FM
26 May 2025, 4:18 pm

Imezoeleka kuwa nyuki hutupatia asali pekee,lakini nyuki hawa wana maziwa yanayopatikana kwa bei ya juu sana,Shirika la Floresta Tanzania wameweza kutubainishia hayo.
Na Elizabeth Mafie-Moshi Kilimanjaro
Wafugaji wa nyuki mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na mazao ya nyuki ikiwemo maziwa na asali ili kuongeza kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Tanzania inatajwa kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa asali duniani, ikizalisha takribani tani 38,000 kwa mwaka, ikitanguliwa na Ethiopia ambayo huzalisha tani 50,000 kwa mwaka.
Miongoni mwa bidhaa zenye thamani kubwa zitokanazo na nyuki ni maziwa ya nyuki, ambapo lita moja ya maziwa hayo huuzwa kwa zaidi ya Sh12 milioni katika baadhi ya masoko ya kimataifa.
Akizungumza Mei 24, 2025 na wafugaji wa nyuki mkoani Kilimanjaro, Ofisa mazingira kutoka Shirika la Floresta Tanzania, Judith Makange, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki na kutumia mbinu za kisasa katika uzalishaji.
Amesema maziwa ya nyuki hupatikana kwa njia ya kitaalamu na si rahisi kama ilivyo kwa asali, lakini bei yake katika soko ni ya juu sana.
Makange amesema kuwa upatikanaji wa maziwa ya nyuki bado ni mdogo kutokana na ugumu wa kuyavuna na kwamba inahitaji kuwa na idadi kubwa ya mizinga ya nyuki kwa ajili ya uzalishaji wake na hivyo kutoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Akizungumza Mkurugenzi wa Shirika la Floresta Tanzania, Richard Mhina amesema tayari wameanzisha vikundi 25 vya ufugaji wa nyuki katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro lengo likiwa ni kuboresha ikolojia na kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia mazao yanayopatikana kwa nyuki ikiwemo, maziwa ya nyuki, asali, nta na mengine mengi.
Amesema shirika hilo lemetoa mtaji wa mizinga minne kwa kila kikundi pamoja na elimu ya namna bora ya ufugaaji wa nyuki na uvunaji wa mazao yake ili kuwezesha wananchi kujiongezea kipato.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha hilo linakuwa endelevu, wanawapa wananchi elimu ya namna ya kuhakikisha wao wanaendelea kuzalisha mizinga mingine na mazao ya nyuki na hata watakapoondoka kwenye usimamizi na ufuatiliaji, waweze kuendelea na ufugaji huo na kupata mafanikio zaidi kwa kizazi cha sasa na baadaye.